2715; Meza yenye mguu mmoja.

Ili meza iweze kuwa imara na kubeba vitu, lazima iwe na miguu zaidi ya miwili.

Meza yenye mguu mmoja au miwili, hata iwe kubwa na imara kiasi gani, haiwezi kustahimili kubeba mzigo mkubwa.

Miguu mingi ndiyo inaipa meza usawa wa kuweza kubeba vitu vingi na kwa utulivu mkubwa.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha ya mafanikio.
Mafanikio siyo kwenye eneo moja tu la maisha, bali kwenye maeneo yote muhimu.

Watu wengi hukazana na eneo moja pekee, wanapata mafanikio makubwa lakini bado wanaishia kuanguka vibaya.

Wanakuwa hawajawa na usawa kwenye maeneo mengine ambayo ni muhimu sana kwenye maisha ya mafanikio.

Fedha, afya, imani na mahusiano ni maeneo ambayo ni muhimu sana kuendelezwa kwa usawa kwenye maisha ya mtu.
Lolote litakaloachwa nyuma kwenye hayo litakuwa na madhara kwa kubomoa mafanikio ambayo mtu anakuwa ameyajenga kwa nguvu kubwa.

Hatua ya kuchukua;
Nenda sambamba na maeneo yote muhimu kwako kwa wakati mmoja.
Usipuuze au kusubirisha lolote, kwani madhara ya kufanya hivyo ni makubwa sana katika kubomoa mafanikio unayokuwa umeyajenga.
Fedha, afya, imani na mahusiano ni vitu unavyopaswa kwenda navyo kwa pamoja ili kuwa na mafanikio yaliyo imara na yatakayodumu.

Tafakari;
Kufanikiwa kwenye jambo moja ni rahisi, wengi hufanya hivyo ila mafanikio hayo hayadumu. Yakipata mtikisiko kidogo yanavunjika kabisa.
Kuwa na mlinganyo sahihi kwenye maeneo yote muhimu siyo kitu rahisi, ni wachache wanaoweza kukamilisha hilo na kujenga mafanikio yanayohimili kila mitikisiko na kudumu kwa muda mrefu.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining