2719; 16/6/50.
Kwenye kurasa mbili zilizopita tumejifunza umuhimu wa kuwa na nidhamu bora ya kazi pamoja na kuendelea kukua binafsi.
Pia tumeona dhana ya kiwango cha muda ambacho mtu unaweka, kuanzia nusu muda, muda kamili na muda wote.
Katika mjadala wa mambo hayo, wengi wamekiri wazi kwamba walikuwa wanadhani wana nidhamu ya kazi na kuweka muda wa kutosha, lakini baada ya kujifunza kwenye kurasa hizo, wamejiona kama wamekuwa wanacheza.
Ukurasa huu ni wa ushauri wa jinsi ya kutenga muda wa kutosha kwa kazi na maendeleo binafsi ili uweze kuwa na nidhamu bora kabisa ya kazi.
Kanuni rahisi ambayo tunaitumia kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni 16/6/50.
Namba ya kwanza ni 16, ambayo ni masaa ya kuweka kazi kwenye siku yako.
Tenga masaa 16 kwenye siku ambayo utayatumia kwenye kuweka juhudi na kujifunza kila siku.
Usizidishe muda zaidi ya hapo kwani utaathiri siku nyingine.
Kuwezesha hilo unapaswa kuianza siku yako mapema kuliko wengine ili kupata muda tulivu wa kufanya yake muhimu.
Kwa mfano ukianza siku yako saa 10 kamili alfajiri na kuimaliza saa nne usiku, hapo kuna masaa 18.
Katika hayo masaa 18, 16 yanapaswa kuwa ya kazi kweli kweli na 2 ndiyo mambo mengine yote kwenye siku yako kama kula, kupumzika, kujenga mahusiano na wengine na n.k.
Masaa 6 kati ya saa nne usiku mpaka saa 10 alfajiri yanakutosha kabisa kulala kama utayatumia vizuri.
Masaa 16 ya kazi yanakuwa ni ya kuweka juhudi kweli kweli, hapo huhesabii kingine chochote, isipokuwa muda wa kujifunza ambao haupaswi kupungua masaa 2 kwenye siku yako hiyo.
Namba ya pili ni 6, ambayo ni siku za kufanya kazi kwenye wiki yako.
Kwa kuwa unaweka kazi kweli kweli kwenye kila siku yako, ni dhahiri mwili wako utajenga uchovu ambao ukienda nao kwa muda mrefu utakukwamisha.
Kuepuka hilo, siku moja kwenye wiki unapaswa kuifanya kuwa siku ya kupumzika.
Kwenye hiyo siku hufanyi kazi kabisa kama siku nyingine.
Bali inakuwa siku maalumu kwa ajili ya kujifanyia tathmini na kuweka mipango ya wiki inayofuata.
Ni siku ya kupata mapumziko ambayo yatafidia uchovu wa siku 6 ambazo zimepita.
Wengi hudhani kwa kufanya kazi siku zote ni kupata muda zaidi, lakini kinachotokea ni kupunguza ufanisi.
Chagua siku moja ya wiki itakayokuwa ya mapumziko kwako na ilinde kweli ili uweze kupumzika.
Namba ya tatu ni 50, ambayo ni wiki za kufanya kazi kwa mwaka.
Mwaka huwa una wiki 52, wewe chagua kufanya kazi kwa juhudi kubwa kwenye wiki 50 za mwaka kisha kuwa na mapumziko ya wiki 2.
Mapumziko hayo yanahusisha kusafiri kwa ajili ya kwenda maeneo ambayo utakuwa na mapumziko ya kweli na hutajihusisha na kazi.
Hapa pia watu huona kujipa likizo ni kupoteza muda, lakini ni njia ya kuondoa uchovu ambao unakuwa umejikusanya kwa muda mrefu.
Kinachowakwamisha wengi wasiweze kuweka juhudi kubwa na kwa muda mrefu ni uchovu wanaokuwa wamejikusanyia kwa muda mrefu.
Kwa kutenga muda ambao hufanyi kazi na ukapumzika, unaujengea mwili nguvu ya kuweza kuendelea na kuweka juhudi.
Hatua ya kuchukua;
Tengeneza kanuni yako ya 16/6/50.
Amua ni masaa yapi 16 yatakuwa ya kuweka juhudi kwako.
Chagua siku zako 6 za kazi kwa wiki na moja ya kupumzika.
Na amua wiki 50 za mwaka utakazoweka kazi kweli na 2 ambazo utapumzika.
Fuata kanuni yako kwa msimamo bila kuivunja na utaweza kuona matokeo makubwa na ya tofauti.
Tafakari;
Kutumia muda wako wa siku, wiki na mwaka bila ya mpango ndiyo njia rahisi kabisa ya kuupoteza na kushindwa kuutumia vizuri.
Wewe pangilia muda wako na utumie kama ulivyopanga, utaweza kufanya makubwa zaidi.
Ufanisi siyo kutumia muda zaidi, bali kutumia vizuri muda ulionao.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining