2725; Una moto kiasi gani?
Dunia inaendeshwa na moto.
Mwanga wa jua, ambao ndiyo unafanya maisha yote yawezekane hapa duniani unatokana na moto unaoendelea ndani ya jua.
Nyota mbalimbali tunazoziona angani, ni mawe yenye moto na ambayo yapo kwenye kasi kubwa.
Moto unasafisha kila kitu.
Moto unaimarisha vitu.
Moto unateketeza vitu.
Moto ndiyo unasukuma vitu vingi kwenye maisha yetu.
Injini zinatumia moto.
Kupika tunatumia moto.
Kama unataka kufanya makubwa kwenye maisha yako, lazima uwe na moto na pia uwe kwenye kasi kubwa.
Moto unaokuwa nao juu ya kile unachofanya na hata maisha kwa ujumla ndiyo unaokupa msukumo wa kufanya makubwa zaidi.
Kama ambavyo moto halisi unaweza kuteketeza msitu mkubwa,
Moto wa ndani yako unaweza kuteketeza kila aina ya ugumu, changamoto na vikwazo unavyokutana navyo kwenye safari yako ya mafanikio.
Kama hufanyi makubwa, siyo kwa sababu huna uwezo, bali kwa sababu moto umepoa ndani yako.
Ni sawa na kuni au mkaa.
Vikiwa havina moto siyo hatari.
Unaweza kuvishika na visiwe na madhara kwako.
Lakini vikipata moto, vinakuwa hatari, ukivishika vinakuunguza.
Hivyo kama hujawa hatari, kama huwaunguzi watu ni kwa sababu ndani yako umepoa.
Washa na chochea moto na utaangaza pamoja na kuwa hatari.
Hatua ya kuchukua;
Kuwa moto kweli kweli kwenye kile unachotaka kupata au kufikia kwenye maisha yako.
Kuwa na msukumo mkubwa wa ndani ambao hauwezi kukwamishwa na kitu chochote kile.
Hilo litakufanya uwe hatari na uweze kufanya makubwa.
Tafakari;
Moto unaokolea, chochote kinachowekwa kwenye moto huo kinakuwa nishati inayozidi kuuchochea moto huo.
Washa moto wako wa ndani kiasi kwamba chochote unachokutana nacho kwenye maisha kinakuwa kichocheo cha wewe kuendelea kufanya makubwa zaidi na siyo kikwazo.
Moto mkubwa hautishwi au kuzuiwa na chochote.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining