2727; Tengeneza wasiwasi wenye manufaa.
Sisi binadamu mara zote huwa tunakuwa na wasiwasi.
Hata kama mambo yako sawa kabisa, huwa hatukosi kitu kinachotupa wasiwasi.
Tena pale mambo yanapokuwa sawa ndiyo tunakuwa na wasiwasi mkubwa zaidi.
Tukifikiria vipi mambo hayo yakiharibika.
Hata kama hakuna tatizo lolote, huwa tunatengeneza matatizo ya kufikirika ambayo yanatuweka kwenye wasiwasi.
Kwa kuwa wasiwasi ni sehemu yetu, ni vyema tukatengeneza wasiwasi wenye manufaa kwetu.
Wasiwasi unaotusukuma kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yetu.
Na sehemu nzuri ya kufanya hivyo ni kujiwekea malengo makubwa kuliko tulivyozoea.
Chagua chochote ulichonacho sasa kisha zidisha mara 10 na hilo ndiyo linakuwa lengo lako.
Wasiwasi utakaokuwa nao kwenye lengo hilo kubwa utaondoa kabisa wasiwasi mwingine kwenye maisha yako.
Tayari unakuwa na kitu kikubwa kinachokupa wasiwasi kiasi kwamba wasiwasi mwingine mdogo mdogo haupati nafasi kwako.
Uzuri wa wasiwasi huo mkubwa unaokuwa nao unakusukuma kufanya makubwa zaidi.
Tofauti tu na wasiwasi mdogo ambao unaishia kukusumbua na usiwe na tija yoyote kwako.
Hatua ya kuchukua;
Orodhesha mambo yote yanayokupa wasiwasi sasa, yote ambayo yanakunyima usingizi.
Pitia moja moja kwenye hiyo orodha yako na ona yapi ni malengo makubwa ambayo yanaweza kuleta matokeo makubwa kwenye maisha yako.
Kama kuna mengi madogo madogo yanayokupa wasiwasi, chagua moja lenye manufaa utakalolifanya kuwa kubwa zaidi na wasiwasi wake uchukue nafasi ya mengin yote.
Tafakari;
Kupata wasiwasi unaotokana na malengo makubwa uliyonayo kuna manufaa kwako kuliko kusumbuliwa na wasiwasi unaotokana na mambo madogo madogo.
Kwa kuwa hakuna wakati ambao hutakuwa na wasiwasi kabisa, basi tengeneza wasiwasi unaokuwa na manufaa kwako.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining