#SheriaYaLeo (235/366); Wape ambacho hawajakizoea.

Ni asili yetu binadamu kupenda kile ambacho hatuna.
Huwa tunaona maisha ya wengine ni bora kuliko yetu pale wanapokuwa na vitu ambavyo sisi hatuna.

Huwa tunaona kazi au biashara za wengine ni nzuri kuliko zetu.
Tunaona maisha yao ni mazuri kuliko yetu.
Mara zote tunatamani yale ambayo wengine wanayo.
Tunadhani kile ambacho sisi hatuna ndiyo bora zaidi.

Na hata tunapopata kile tunachotamani, bado haturidhiki na kutulia.
Badala yake tunakizoea na kuona ni cha kawaida.
Halafu tunaanza kutamani vingine ambavyo hatuna.

Hivyo ndivyo binadamu tulivyo.
Huwa hatuthamini tulichonacho kama kile ambacho hatuna.

Hivyo unapotaka kuwashawishi watu, wahadae na vitu ambavyo hawajavizoea na hawana.
Kwa kuwafanya watu waone wanaenda kupata kitu cha tofauti na walivyozoea, wanafuatilia kwa umakimi zaidi.

Watu pia huwa wanapenda vitu ambavyo ni mwiko au vimekatazwa.
Na ndiyo maana biashara zozote za magendo huwa zinalipa sana.
Kwa sababu watu wanatamani kupata kile walichokataza au kuzuiwa.

Hiyo ni njia nyingine nzuri ya kuwashawishi watu, kuwafanya waone wanapata kitu ambacho hawawezi kukipata mahali pengine.

Sheria ya leo; Pale tunapokuwa na kitu huwa tunakizoea na kukidharau. Lakini kitu ambacho hatuna na ambacho siyo rahisi kupatikana huwa tunakitamani zaidi. Hivyo ili kuwashawishi watu, waonyeshe wanakwenda kupata kitu ambacho hawana, kitu ambacho hakijazoeleka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji