2732; Kukosa kwako umakini kunakuumiza.
Kiwango chako cha kukosa umakini, kinaiumiza sana biashara yako.
Huo ni ujumbe nilioutuma kwa mmoja wetu baada ya kuona kuna mambo ya msingi kabisa yanamsumbua.
Nilipozungumza naye, nikagundua tatizo ni kubwa kuliko nilivyokuwa nadhani awali.
Na maumivu kwenye biashara yanayosababishwa na kukosekana kwa umakini yalikuwa makubwa.
Injili yetu kuu hapa ni kufanya kazi kwa juhudi kama njia kuu ya mafanikio.
Lakini haijalishi unaweka kazi kiasi gani, kama utakosa umakini, kazi yote unayoweka inakuwa bure.
Juhudi zote unazoweka unaishia kupoteza.
Utaumia sana kwenye kazi, lakini matokeo bado yatakuwa mabovu.
Punda ni mnyama anayefanya kazi sana, lakini hayupo kwenye orodha ya wanyama wenye mafanikio kwa sababu hana umakini.
Ataweka kazi pale anapotumiwa na wengine, lakini siyo akiwa peke yake.
Simba ni mnyama anayefanya kazi muda mfupi kuliko wanyama wengine wote.
Lakini pia ndiyo mnyama mwenye mafanikio makubwa.
Hiyo ni kwa sababu ana umakini mkubwa.
Akishaweka lengo lake kwenye kupata kitoweo, hapotezi muda na nguvu kwenye vitu vingine.
Anawinda mpaka apate kitoweo.
Sasa hebu fikiria wewe utafika wapi kama utakuwa na umakini mkubwa kama wa simba na kufanya kazi kwa juhudi kama punda.
Ndani ya muda mfupi tu utapiga hatua mara mbili ya pale ulipo sasa.
Hivyo kumbuka, siyo kazi pekee itakayokulipa, bali pia na umakini mkubwa kwenye kila unachofanya.
Haina maana kufanya kwa juhudi kitu ambacho hukupaswa kukifanya kabisa.
Ni upotevu wa nguvu na muda, vitu ambavyo huwezi kuvipata tena.
Haina maana kukazana kujaza pipa la maji ambalo linavuja.
Utaweka juhudi usiku na mchana na bado halitajaa, kwa sababu japo unaweka, bado pia unapoteza.
Tuweke kazi kwa juhudi pamoja na kuwa na umakini mkubwa, kitu ambacho kitatupa matokeo makubwa na bora zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Angalia ni maeneo gani ambayo licha ya kuweka juhudi kubwa bado hupati matokeo. Kwenye maeneo hayo kuna umakini umekosekana.
Pambana kuongeza umakini wako kwenye maeneo hayo ili uweze kufurahia matunda ya juhudi kubwa unazoweka kwenye kazi.
Tafakari;
Kila mtu anafanya kazi, bila ya kujali kwa kiwango gani.
Kama kila mtu angeweka umakini mkubwa kwenye kazi anayofanya, hata kama anaifanya kwa kiwango cha kawaida, bado ataweza kupata matokeo makubwa.
Kukosa umakini kunawaumiza wengi kuliko kiwango cha kazi wanachoweka.
Wewe fanya kazi kwa juhudi kubwa na kuwa na umakini wa hali ya juu.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WorkHardAndYouWillSucceed
#We’reAllGonnaMakeIt