2733; Hakuna kukosea.
Kipindi cha nyuma kidogo palikuwa na kichekesho kwamba kulikuwa na bendi ya waimbaji ambao walikuwa wanasafiri kwenda kutoa burudani.
Mmoja wa wanamuziki akawa amechomwa na msumari ndani ya gari waliyokuwa wanasafiria.
Kwa kuwa aliyechomwa alikuwa muimbaji, aliamua kumwambia dereva kwamba amechomwa na msumari, lakini akamwambia kama vile anaimba.
Wenzake kusikia hivyo wakadhani ni wimbo mpya amekuja nao, hivyo wakaanza kuimba wote kwa pamoja.
Kuna uvumbuzi mwingi sana duniani ambao ulitokana na makosa.
Kwa mfano hata dawa tunazotumia (antibiotics) ziligunduliwa kimakosa.
Mtafiti alikosea kuacha fangasi kuingia kwenye eneo ambalo bakteria walikuwa wamepandikizwa.
Na hilo eneo ambalo fangasi waliingia, bakteria hawakuota.
Ndiyo akagundua kwamba fangasi wana uwezo wa kuua bakteria.
Kuna makampuni ambayo yalianza na lengo la kuzalisha bidhaa mpya, lakini ikakosewa. Ila bidhaa hiyo iliyokosewa ikawa na manufaa mengine makubwa zaidi na kuinufaisha sana kampuni.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaishi maisha yako, kwa kila unachokosea, usiishie tu kuumia na kujilaumu.
Badala yake jiulize makosa yako yanawezaje kuwa na manufaa makubwa kwako?
Kwanza kabisa ni kuyatumia kama sehemu ya kujifunza ili usiyarudie tena. Kurudia kosa lile lile zaidi ya mara moja ni uzembe wa hali ya juu.
Pili ni kuangalia kama matokeo ya makosa uliyofanya yanaweza kuwa na matumizi yenye tija zaidi.
Usiishie tu kujilaumu kwa makosa uliyofanya, badala yake angalia kama yanaweza kutumika kwa manufaa.
Mara zote tambua hakuna kukosea,
Kuna kujifunza na kuwa bora zaidi.
Hivyo usirudie kosa moja mara mbili.
Na matokeo ya kila kosa yatumie kwa namna bora zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Pitia makosa yote ambayo umewahi kufanya kwenye maisha yako na yakaishia kuwa na manufaa kwako.
Hilo likufanye ujue hakuna kukosea, badala yake kuna kujifunza na kuwa bora zaidi.
Unakosea pale tu unapofanya kitu kile kile zaidi ya mara moja.
Tafakari;
Huwa wanasema kila mtu anakosea, lakini hiyo siyo kweli sana, wanaoyatumia makosa yao kwa manufaa hawakosei, badala yake wanajifunza na kuwa bora.
Wanaorudia makosa yale yale ndiyo wanakuwa wazembe na wanaodhurika.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#We’reAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed