#SheriaYaLeo (237/366); Changanya ukali na wema.
Unapokuwa kiongozi unahitaji sana kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine ili kuweza kuwaongoza vizuri na kufanya makubwa.
Njia bora ya kufanya hivyo ni kuchanganya ukali na wema.
Na hilo unalifanya kupitia zawadi na adhabu unazozitoa.
Kama kiongozi unapaswa kueleza taratibu za watu wako kufuata.
Pale wanapofanya vizuri unawapa zawadi na pale wanapofanya vibaya unawapa adhabu.
Lakini sasa, zawadi na adhabu vinapaswa kuwa kwa nadra, kwani vikitolewa kwa wingi watu wanazoea na vinaacha kuwa na nguvu.
Zawadi zikitolewa kwa wingi watu hawazioni kama kitu cha thamani, hivyo hawasukumwi kufanya vizuri ili kuzipata.
Na adhabu zinapotolewa kwa wingi watu wanazizoea na hawaziogopi tena.
Pale vitu hivyo vinapokuwa kwa nadra, vinakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.
Zawadi zinapokuwa kwa nadra zinathaminiwa, watu wanasukumwa kuwa bora ili wapate zawadi.
Na adhabu zinapokuwa nadra watu wanazihofia na kukazana kuzikwepa.
Unapotoa zawadi, inapaswa kuwa zawadi bora kweli inayowafanya wengine wengi kutaka kuipata hivyo kufanya yaliyo sahihi.
Na pia unapotoa adhabu, inapaswa kuwa adhabu kali kweli inayowafanya wengine wahofie kupata adhabu hiyo.
Matumizi mazuri ya zawadi na adhabu yatakujengea ushawishi mkubwa kwa wale ambao unawaongoza. Kwani wakishajua vitu gani vinakufurahisha na vipi vinakuudhi watakazana kwenda kwa namna sahihi.
Sheria ya leo; Waweke watu kwenye hali ya kutokuwa na uhakika, wakikufikiria kwa muda mrefu na wakitaka kukuridhisha. Tumia zawadi na adhabu kwa nadra na kwa nguvu kubwa ili kuwashawishi watu waende vile unavyotaka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji