2740; Wanataka kukutumia.
Baadhi ya mambo ambayo tumekuwa tunajifunza kuhusu binadamu ni ubinafsi na maslahi.
Huwa tuna ubinafsi mkubwa na kujali zaidi maslahi yetu wenyewe.
Na hilo ndiyo linawafanya watu kuwa tayari kuwatumia wengine pale wanapoona kuna maslahi mazuri kwa ajili yao.
Hivyo lazima ujue kwenye mahusiano yako mengi na watu wengine, mengi yanakuwa yameegemea kwenye manufaa.
Watu wanakuwa karibu zaidi na wewe pale wanapoona fursa ya kukutumia ili wapate kile wanachotaka.
Wakishapata wanachotaka au wakiona hawawezi kukipata tena kutoka kwako, wanakuwa hawaoni sababu ya kuendelea kuwa na wewe.
Kwa kuelewa hili hupaswi kuwachukia watu kwa sababu wanakutumia.
Badala yake unapaswa kujifunza jinsi ya kuhusiana naye bora, kwa namna ambayo kila upande unanufaika.
Na wakati mwingine, njia bora ya kunufaisha pande zote ni kusitisha mahusiano au ushirikiano ulionao na wengine.
Unafanya hivyo pale unapogundua upande mmoja una utegemezi mkubwa kwenye upande wa pili.
Yaani manufaa yanakuwa zaidi kwenye upande mmoja kuliko upande mwingine.
Hatua ya kuchukua;
Pitia mahusiano na ushirikiano wote ulionao na watu wengine. Jiulize wewe unanufaikaje na mahusiano na ushirikiano huo. Pia angalia wale unahusiana na kushirikiana nao wananufaikaje.
Kama kuna upande ambao haunufaiki au unaumia kwenye mahusiano na ushirikiano huo, ni wakati wa kupitia upya.
Tafakari;
Watu wanaotaka kunufaika kupitia wewe, huwa wanakuweka kwenye hali na mazingira ya kukudhibiti na kukufanya uone bila ya wao wewe huwezi.
Unachopaswa kujua ni kwamba wanakushikilia kwa sababu una manufaa kwao.
Ina maana ukiwa huru, unaweza kufanya makubwa zaidi.
Kamwe usikubali wengine wakudhibiti na kukutumia kama wanavyotaka wao.
Hakikisha unajenga mahusiano na ushirikiano ambao pande zote mbili zinanufaika.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed