#SheriaYaLeo (245/366); Fikiria zaidi ya pale ulipo sasa.

Kwenye vita, mkakati ni sanaa ya kudhibiti mpango mzima wa kivita. Wakati mbinu ni ujuzi wa kukabiliana na pambano lililo mbele yako.

Wengi wetu kwenye maisha ni watu wa mbinu badala ya mikakati.
Tunavurugwa na yale yanayoendelea kwa wakati huo kiasi kwamba tunashindwa kufikiria zaidi ya pale tulipo sasa.

Kufikiri kimkakati ni kugumu na siyo asili yetu binadamu.
Unaweza kudhani wewe ni mtu wa mikakati, lakini ukawa ni mtu wa mbinu zaidi.

Ili uweze kupata nguvu ambayo mikakati pekee ndiyo inaweza kukupatia, ni lazima uweze kufikiri zaidi ya kile kinachoendelea sasa.
Ni lazima uweze kuona makubwa zaidi ya yale yanayokukabili kwa sasa.

Mara zote fikiria kuhusu maono na ndoto zako kubwa badala ya kuvurugwa na changamoto unazopitia kwa wakati husika.
Ni maono na ndoto zako kubwa ndiyo vitakuongoza nini ufanye na nini usifanye.
Itakusaidia kuamua ni vita gani upigane na ipi uachane nayo.

Kwa kuwa na mkakati bora, ni rahisi kuwa na mbinu zinazokupa matokeo mazuri.
Lakini kukosa mikakati na kutegemea mbinu pekee ndiyo chanzo cha kushindwa kwenye mambo makubwa.

Sheria ya leo; Watu wa mbinu huwa ni wazito na wasioona mbali, wakati watu wa mkakati ni wepesi na wanaoona mbali. Je wewe upo upande gani?

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji