2744; Usichoambiwa kuhusu mauzo.
Kitu kimoja ambacho watu wengi huwa hawaelewi kwa uhalisia kwenye mauzo ni kwamba mara nyingi wateja huwa wanakudanganya.
Na wanafanya hivyo kwa nia njema kabisa ya kutokutaka kukuumiza.
Lakini wanaishia kukuumiza zaidi kwa kutokununua kwako.
Mapingamizi mengi ambayo mteja anakupa siyo halisi, hasa kwenye pingamizi la bei.
Na ahadi nyingi mteja anakupa huwa hamaanishi, ni njia tu ya kukuhama.
Huwa kuna kichekesho kinasema kama wateja wote wanaokuambia watarudi wangekuwa wanarudi kweli, basi biashara zingefanikiwa sana.
Ukweli ni wateja watakuahidi wanarudi na kila mtu anajua hawatarudi.
Lakini tunajikuta tukikubaliana nao.
Kwa sababu hatukuwa tumejipanga kuwauzia.
Leo nakwenda kukushirikisha mabadiliko ya kimtazamo ambayo yatakusaidia kuwauzia wateja zaidi bila ya kudanganywa.
Mtazamo unaopaswa kuwa nao ni kwamba kila mteja anayekuja kwenye biashara yako, au anayepiga simu kuulizia basi tayari ana uhitaji.
Unatambua kuna watu wengi ambao wanapita eneo la biashara yako kila siku ila hawajisumbui kuulizia, kwa sababu hawana uhitaji.
Kwa maana hiyo basi, yule anayeacha mambo yake na kuja kwenye biashara yako, kuna uhitaji ambao tayari anao.
Kuna wengine wengi ambao wanakutana na matangazo yako kila siku, lakini hawapigi simu kuulizia, kwa kuwa hawana uhitaji.
Hivyo inapotokea akawepo aliyepiga simu, kuna uhitaji umemsukuma kufanya hivyo.
Kile ambacho mteja anafanya ndiyo ukweli na siyo kile anachokuambia.
Na ukweli ni amekuja kwenye biashara yako, au amepiga simu, hivyo ana uhitaji.
Wajibu wako ni wewe kuhakikisha unampatia mteja huyo uhitaji wake.
Kutokupokea kirahisi sababu nyingine anazotumia kukutoroka.
Muulize mteja maswali zaidi, msikilize kwa makini na jibu maswali na mapingamizi yake yote.
Nenda na mteja mpaka pale anapokuwa amejenga imani kwako na kuwa tayari kununua.
Hilo linahitaji kazi na muda, na kwa kuwa upo kwenye biashara, basi ifanye hiyo kuwa sehemu ya kazi yako, mchakato kamili wa mauzo.
Hatua ya kuchukua;
Mteja yeyote anayefika kwenye biashara yako au kupiga simu, jiambie tayari anao uhitaji. Wajibu wako ni kuhakikisha unajua uhitaji wake na kuweza kuutimiza.
Usikubali kupokea sababu na mapingamizi yasiyo ya kweli.
Tafakari;
Wateja huwa wanadanganya, kwa nia njema kabisa kwa upande wao. Ila nia hiyo njema kwao inaishia kuwa na maumivu kwetu.
Ni wajibu wetu kama wauzaji kuhakikisha hatukubali kirahisi hilo, kwa kuyaangalia matendo ya mteja na kuyatumia hayo kuhakikisha ananunua.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed