2747; Uongozi ni maono na msimamo.

Mengi husemwa na kufundishwa kuhusu uongozi.
Sifa nyingi hutajwa kwenye uongozi.
Lakini kuna sifa kuu mbili zinazohitajika sana kwenye uongozi ili uweze kuwa na manufaa.
Sifa hizo ni maono na msimamo.

Kiongozi lazima awe na maono makubwa ya siku zijazo na ambayo anaamini kabisa yatafikiwa, japo kwa sasa yanaonekana kutokuwezekana.
Hii ni sifa muhimu sana kwa kiongozi kuwa nayo kwa sababu watu wengi huwa hawana maono makubwa na hata wakiwa nayo huwa hawayaamini hivyo hawathubutu kuyasema.
Lakini watu hao hao wanaposikia kuna mtu ana maono makubwa, huwa tayari kumfuata.
Hivyo unapokuwa na maono makubwa kama kiongozi, hutengenezi wafuasi wenye maono makubwa, bali unawavuta kuja kwako.
Watu hao wenye maono makubwa tayari wapo, ila wanakuwa hawajapata mtu ambaye ana maono makubwa na anayaamini.

Sifa ya pili ni msimamo katika kuyaendea maono hayo makubwa.
Watu wengi huwa wanakuwa na maono makubwa, ambayo yanawapa hamasa kubwa mwanzoni.
Hamasa hiyo inawasukuma kuanza kuchukua hatua mara moja kwenye maono hayo.
Lakini baada ya muda, hamasa ile inaisha na hawaendelei tena.
Badala yake wanatafuta kitu kingine kipya cha kuhangaika nacho.
Kiongozi bora ni yule anayeendelea kuyasimamia maono yake mpaka yanapofikiwa.
Haijalishi anapitia nini, hakubali kutetereka kwa namna yoyote ile.
Anahakikisha watu wake wanakaa kwenye maono hayo bila ya kutekwa na vitu vingine vipya.
Ni kwa njia hiyo ndiyo viongozi hao huweza kufanya makubwa ambayo yameshindikana na wengine.

Kuwa na maono makubwa na kuyasimamia bila ya kutetereka ni sifa kuu mbili ambazo ukiwa nazo kwa uhakika, utashangaa jinsi ambavyo watu sahihi watakuja kwako na utaweza kushirikiana nao kufanya makubwa.

Hatua ya kuchukua;
Je unazo sifa hizi kuu mbili za uongozi? Jipime kwa maswali haya;
1. Ni maono gani makubwa uliyonayo, ambayo unaamini utayafikia licha ya kuonekana hayawezekani kwa sasa?
2. Ni msimamo kiasi gani unao kwenye maono hayo na unaepukaje kuchoka au kutekwa na mambo mengine mapya?
Jibu maswali hayo mawili kujipima kiuongozi na mafanikio.

Tafakari;
Uongozi siyo cheo anachopewa mtu, bali namna anavyochagua kuyaishi maisha yake.
Kuna watu wana vyeo vya uongozi ila tabia zao ni za ufuasi, hawa huwa hawapati mafanikio makubwa.
Na kuna watu ambao hawana vyeo vya uongozi ila wana tabia za uongozi, hawa kupata mafanikio makubwa.
Usisubiri cheo au wafuasi, wewe kuwa na tabia za uongozi na mengine yatafuata.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed