2754; Muda wa kazi na muda unaofanya kazi.

Hakuna eneo ambalo watu wengi huwa wanajidanganya kama kwenye muda.
Na usipokuwa mkweli kwenye muda wako mwenyewe, hakuna namna unaweza kufanikiwa.

Watu wawili, wanaweza kufanya kitu cha aina moja na kuonekana wakiwa na muda unaolingana.
Bado mmoja akafanikiwa zaidi ya mwingine.

Tofauti kubwa huwa inaanzia kwenye matumizi yao ya muda.
Wote wanaweza kuwa wametenga muda unaolingana wa kufanya kitu.
Lakini jinsi wanavyotumia muda huo ndiyo wakatofautiana.

Muda wa kazi ni ule muda ambao ndiyo unautenga kwa ajili ya kazi zako.
Ni muhimu kutenga muda huo ili uweze kupangilia vyema vipaumbele vyako.

Lakini kama tunavyojua, mipango siyo matumizi. Pamoja na kupanga muda wa kazi, huwa siyo muda wote mtu unautumia kufanya kazi.
Kwa wengi, sehemu kubwa ya muda wa kazi huwa wanaitumia kwenye mambo yasiyohusu kazi yao.
Wanamaliza siku wakiwa wamechoka, lakini hakuna chochote cha tofauti wanachokuwa wamezalisha.

Na hapo ndipo tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa inapoanzia.
Wanaofanikiwa wanapanga muda wa kazi na kutumia muda huo kwenye kazi tu. Wanakuwa na vipaunble sahihi kwao na kuvisimamia.

Kwa upande wa pili, wasiofanikiwa huwa wanapanga muda wa kazi, lakini wanatumia muda huo kufanya mambo yasiyohusiana na kazi.
Hawana vipaumbele sahihi kwao, badala yake wanarukia kila linalokuja mbele yao, kitu kinachowachosha na wasizalishe matokeo ya tofauti.

Hatua ya kuchukua;
Leo jikague ni muda kiasi gani ambao umetenga kwa ajili ya kazi. Kisha angalia katika muda huo uliopanga, ni kwa asilimia ngapi unatumia muda huo kwenye majukumu ya kazi?
Kadiri unavyoweka muda wako wa kazi kwenye kutekeleza majukumu muhimu ya kazi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo bora zaidi.

Tafakari;
Kinachokupa mafanikio siyo muda unaopanga kufanya kazi. Bali jinsi unavyotumia muda huo wa kazi.
Kama unaruhusu mambo yasiyohusu kazi kuingia kwenye muda wako wa kazi, unajizuia kufanikiwa.
Ukishatenga muda wa kazi, utumie muda huo kwenye mambo yanayohusu kazi peke yake.
Mengine yasiyohusu kazi hayapaswi kupata nafasi kwenye muda wako wa kazi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed