2757; Kuwepo na kutumika.

Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa siyo kuwepo au kutokuwepo kwa vitu fulani, bali kutumika au kutokutumika kwa vitu hivyo.

Kwa mfano wale waliofanikiwa huwa wanatumia uwezo mkubwa ulio ndani yao.
Hiyo haimaanishi kwamba wanaoshindwa hawana uwezo mkubwa ndani yao.
Wanao sana, ila kinachowakwamisha ni kutokuutumia.

Na mara nyingi hawautumii kwa sababu hakuna kinachowasukuma kufanya hivyo.

Twende na mfano ili tuelewane vizuri.
Nikikuambia sasa hivi upande ukuta mrefu kwa haraka utasema huwezi.
Lakini ikitokea unakimbizwa na mbwa mkali, utapanda ukuta huo kwa haraka sana.
Je nini kimebadilika hapo?
Kukimbizwa na mbwa hakujaongeza uwezo wowote ndani yako, bali kumekulazimisha utumie uwezo ambao tayari upo ndani yako.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio.
Kila unachohitaji tayari kipo ndani yako.
Lakini ili uweze kukitumia lazima kwanza uwe na hasira kali na kubwa, uwe na msukumo ambao haukuachi ukatulia.

Ndiyo maana mara nyingi watu hupata mafanikio makubwa pale wanapokuwa na hasira kubwa juu ya kitu fulani.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni kitu gani kinachoweza kukusukuma wewe kutumia uwezo mkubwa ambao tayari upo ndani yako?
Ni kitu gani kinachokupa hasira sana ambapo upo tayari kujisukuma kwa kila namna ili kukikabili?
Tafuta sababu ya kulazimika kutumia uwezo wako wote mkubwa ulio ndani yako.

Tafakari;
Kila mtu tayari anao uwezo mkubwa na wa tofauti ulio ndani yake. Ila kuweza kufikia na kutumia uwezo huo ndiyo sehemu ambayo watu wanatofautiana.
Bila ya kuwa na sababu inayokusukuma kufikia na kutumia uwezo wako mkubwa wa ndani, utaishia kubaki ukiwa umelala ndani yako.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed