2758; Ni asilimia 75.
Aisee, kujifunza hakuna mwisho na hakuna wakati unaweza kusema umeshajua kila kitu, hata vitu vya msingi kabisa.
Kwa mfano kwenye eneo la fedha binafsi, tumekuwa tunajifunza msingi mkuu wa kujenga utajiri na uhuru wa kifedha ni kujilipa mwenyewe asilimia 10 ya kila kipato unachoingiza.
Hilo linajulikana wazi na kila mmoja na ndiyo msingi mkuu.
Siku za karibuni niliingia kwenye mtandao wa YouTube kuangalia somo fulani, kwa pembeni nikaona kichwa cha somo jingine fupi kinachosema tofauti ya utajiri (rich) na ukwasi/uhuru wa kifedha (wealthy).
Mnenaji alisema kwa lugha nyepesi kabisa kwamba utajiri ni kitu ambacho kinaishia kwako wewe mwenyewe. Wakati ukwasi unakwenda kwa vizazi na vizazi.
Alieleza kwamba watu wengi wanapolipwa fedha huwa wanatumia zote kisha kwenda kutafuta nyingine.
Lakini wanaopata utajiri huwa wanaweka akiba kwenye kila kipato.
Mpaka hapo sikuona chochote kipya.
Ni kile alichoendelea kusema ndiyo kilinifungua zaidi.
Alisema wanaofikia utajiri huwa wanaweka nusu ya kipato chao akiba na kisha kuwekeza, wanatumia nusu tu.
Hapa nilianza kufikiria kidogo kuhusu kuweka asilimia 10. Nikaona bado ni chini ukilinganisha na hiyo asilimia 50.
Kilichonimaliza kabisa ni pale mnenaji aliposema wanaofikia ukwasi wanaenda zaidi ya hapo, wanaweka akiba robo tatu ya kipato chao. Yaani asilimia 75 wanaiweka pembeni na kutumia asilimia 25 pekee.
Ni kiwango hicho kikubwa wanachoweka pembeni na kuwekeza ndiyo kinawafikisha kwenye uhuru wa kifedha.
Hili lilinifanya nifikiri sana kwa kina na nikaona kama safari ya utajiri na ukwasi ni mchezo wa mpira, basi kuna ngazi tano.
Ngazi ya kwanza ni ya utazamaji, hapa haupo kabisa kwenye mchezo, yaani huweki akiba yoyote, unatumia chote unachopata.
Ngazi ya pili ni ligi ya mchangani, yaani ile michezo ya mitaani. Hapa ni pale unapoweka akiba asilimia 10 ya kila kipato chako.
Ngazi ya tatu ni ligi daraja la kwanza, hapa unaweka akiba asilimia 50 ya kila kipato chako.
Ngazi ya nne ni ligi kuu, hapa unaweka asilimia 75 ya kipato chako.
Na ngazi ya juu na ya mwisho ni ligi ya mabingwa, hapa unaingiza kipato ambacho unaweza kuweka akiba kwa asilimia 100 bila kuathiri maisha yako. Yaani unakuwa umefikia uhuru wa kifedha.
Swali muhimu la kujiuliza ni upo kwenye ngazi ipi au unacheza ligi gani?
Hatua ya kuchukua;
Pitia upya mkakati wako wa kufikia uhuru wa kifedha na kiwango ulichokuwa umejiwekea kwenye kuweka akiba na kuwekeza.
Angalia kama kinakuweka kwenye ngazi sahihi au unapaswa kubadili ili kwenda kwenye ngazi sahihi itakayokufikisha kule unakotaka kufika.
Tafakari;
Ni kipato kiasi gani unachopaswa kuingiza ili uweze kucheza ligi kuu? Yaani unapaswa kuingiza kipato kiasi gani ili uweze kuweka akiba asilimia 75 bila kuathiri maisha yako?
Hiyo ndiyo namba muhimu unayopaswa kuanza kuifanyia kazi mara moja ili kufikia uhuru wa kifedha.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed