2759; Ninakuhitahu zaidi wakati una matatizo.

Kitu kimoja ambacho nimeendelea kujifunza kwenye huduma ya ukocha ninayotoa ni pale ambapo watu wanaihitaji zaidi huduma yangu ndipo wanaikimbia.

Pale mtu anapojikuta kwenye matatizo na changamoto kubwa, ndiyo unapaswa kuwa wakati mzuri kwake kutumia huduma ya ukocha kuvuka hilo.

Lakini badala yake wengi ndiyo wanaikimbia huduma kwa wakati huo.
Wakisema hawaihitaji mpaka pale watakapomaliza matatizo yao.

Yaani ni sawa na mtu mwenye njaa aseme hahitaji chakula mpaka pale njaa itakapokuwa imeisha!
Ni jambo la kushangaza, una njaa, chukula kipo mbele yako, lakini unakikataa mpaka njaa iondoke.
Unadhani hiyo njaa itaondokaje?

Unahitaji zaidi huduma ya ukocha pale unapokuwa na matatizo na changamoto mbalimbali kwenye maisha yako.
Huo ndiyo wakati unapohitaji sana mtu wa kushirikiana naye kwa karibu katika kuzivuka.

Hata kama mtu huyo hatabeba matatizo na changamoto hizo moja kwa moja, bado uwepo wake utakupa fursa ya kuona mambo kwa uhalisia wake.

Iko hivi, mara nyingi unapokuwa kwenye matatizo na changamoto mbalimbali, yananasa zaidi hisia zako.
Kitu ambacho kinaathiri zaidi maamuzi unayofanya.
Ndiyo maana ni rahisi kutengeneza matatizo zaidi pale unapokuwa tayari upo kwenye matatizo.
Yote hiyo inatokana na hisia zinazokuwa zimekutawala kwenye wakati huo.

Unapokuwa na mtu ambaye haangalii hali hiyo kwa hisia, anakusaidia kuona uhalisia na kuweza kufanya maamuzi sahihi. Hiyo itapunguza kutengeneza makosa zaidi.

Hakuna mtu anayehitaji huduma ya ukocha kwenye kuyafurahia maisha, tayari kila mtu ni mbobezi kwenye hilo.
Ni wakati wa magumu na changamoto mbalimbali ndiyo kila mmoja anahitaji sana huduma ya ukocha.
Lakini kwa bahati mbaya, ndiyo wakati ambao wengi wanazikimbia huduma za aina hiyo.

Mimi kama kocha wako, nakuhitaji sana pale unapokuwa na matatizo na changamoto mbalimbali.
Kwani hapo ndipo tunaweza kufanya kazi kwa pamoja, ukayavuka hayo na kubaki ukiwa imara zaidi.
Usikimbie katika wakati huo ambapo unahitaji mno huduma hiyo.
Na wala usione kama ni usumbufu, hakuna kitu ambacho kocha yeyote anakipenda kama matatizo na changamoto.

Hatua ya kuchukua;
Unapojikuta kwenye matatizo na changamoto mbalimbali ndiyo wakati mzuri wa kufanya kazi kwa karibu na kocha.
Na kama huna matatizo au changamoto unazopitia, ni kiashiria kwamba unacheza mchezo mdogo sana, unacheza salama na itakuwa vigumu kupata mafanikio makubwa.
Hivyo anza kwa kujitengenezea matatizo au changamoto ambazo zitakufanya uhitaji sana huduma ya ukocha na hapo fanya kazi kwa karibu na kocha ili upige hatua zaidi.

Tafakari;
Kama huna matatizo au changamoto zinazokusumbua sasa na kukufanya uhitaji sana huduma ya ukocha, anza na kipato chako. Chukua wastani wa kipato unachoingiza sasa, kisha zidisha mara 10. Hilo liwe ndiyo lengo la kipato unalotaka kufikia. Kisha fanya kazi kwa karibu na kocha wako ili kuweza kufikia lengo hilo.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed