2761; Unajitofautishaje na wengine?

Unajua ninj rafiki yangu,
Neno siri za mafanikio limewanufaisha sana wengi.
Kuna wengi ambao wameweza kuingiza kipato kikubwa kwa kuwaambia wengine kwamba wanazo siri za mafanikio.

Sasa kwa sababu jamii kwa ujumla haiyaelewi mafanikio, hunasa kwenye huo mtego. Kwa kuamini kutakuwa na siri za mafanikio ndiyo maana wachache ndiyo wamefanikiwa.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna siri kwenye mafanikio.
Kil kitu kipo wazi kabisa.
Sema tatizo kubwa ni wengi hawapo tayari kufanyia kazi yale wanayojua kubusu mafanikio yakawapa matokeo ya tofauti.

Kwa mfano, kama unafanya kile ambacho wengine wanafanya na unakifanya kwa namna ambayo hata wao wanakifanya, utaishia kupata matokeo ambayo wengine wanayapata.
Hakuna muujiza wowote kwenye hilo.

Kwa kujua hili la msingi kabisa, tunarudi kwako na swali muhimu, unajitofautishaje na wengine?
Ni kitu gani cha tofauti unachofanya ambacho wengine hawafanyi?
Au kama wanakifanya, je wewe unakifanyaje kwa utofauti mkubwa?

Hakuna namna utaweza kufanikiwa kama hujitofautishi na wengine.
Hiyo siri, ni jambo ambalo lipo wazi kabisa.
Ambalo kila mtu analijua.
Lakini wengi hawalifanyi.
Kwa sababu hawapendi kusumbuliwa na wengine.

Ipo hivi rafiki,
Pale utakapofanya tofauti na wengine,
Utakuwa umetangaza nao vita.
Kwani wataleta kwako mashambulizi ya kila aina.
Watakuonyesha unakosea na utashindwa.
Kama haupo imara, hayo mashambulizi yatakupoteza kabisa.

Kama kweli umejitoa kufanikiwa,
Kwanza jitofautishe na wengine.
Na pili jiamini na simamia kile kilicho sahihi hata kama utashambuliwa na watu wengi kiasi gani.
Lazima uwajue wale walioshindwa na kukata tamaa na uwaepuke kama ukoma, maana sumu yao ni kali na mbaya.

Hatua ya kuchukua;
Leo jikumbushe ni maeneo gani ambayo umechagua kujitofautisha kabisa na wengine.
Simama kwenye utofauti uliojenga bila ya kukubali kuyumbishwa na kwa njia hiyo ndiyo utaweza kupata matokeo ya tofauti na kufanikiwa.

Tafakari;
Kama hufurahishwi na matokeo unayopata sasa, tayari unajua pa kuanzia, ni kwenye hatua unazochukua.
Kwa kubadili hatua unazochukua utaweza kubadili matokeo unayoyapata.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed