2762; Kujiandaa kuishi.

Watu wengi huwa wanayamaliza maisha yao hapa duniani kabla hata hawajaanza kuishi.

Kila wakati wanakuwa wanajiandaa kuanza kuishi.
Hatimaye mauti yanawafika kabla hata hawajawa tayari kuishi.

Ukifuatilia maisha ya wengi, na huenda hata ya kwako binafsi, hilo lipo dhahiri kabisa.

Wakati mtu akiwa mtoto, anaenda shule kujiandaa kukabiliana na maisha.
Anapomaliza shule anatafuta kazi au biashara ya kumwezesha kuanza maisha.

Akipata kazi au biashara anazitumia kama njia ya kujenga maisha atakayoyaishi.
Anakuwa na familia na majukumu yanaongezeka.
Hapo analazimika kukimbizana na majukumu hayo na kuahirisha kuishi.
Anajiambia akishastaafu au kufika ngazi fulani basi ndiyo ataanza kuishi.

Anaenda hivyo mpaka kufikia kustaafu au ngazi aliyokuwa amepanga, anagundulika ana magonjwa sugu na yasiyotibika kitu kinachompeleka kwenye mauti ndani ya muda mfupi.

Kwa kipindi chote hicho, mtu anakuwa hajayaishi maisha yake, bali alikuwa anajiandaa kuishi.

Zipo kauli mbili muhimu sana zinazoweza kutusaidia kwenye hili.

Kauli ya kwanza inasema; maisha ni kile kinachotokea wakati unaendelea kuhangaika na mambo mengine kwenye maisha yako.
Kwa maana nyingine ni huwezi kujiandaa kuishi, bali maisha yanakuwa yanaendelea, iwe unajua au hujui.

Kauli ya pili inasema; maisha siyo kusubiria mpaka dhoruba ipite, bali ni kujifunza kucheza kwenye mvua.
Kwa maana nyingine ni hakuna wakati ambao kila kitu kitakuwa sawa ndiyo uanze kuishi.
Kila wakati kutakuwa na changamoto unayokabiliana nayo. Hivyo hupaswi kuyaahirisha maisha yako.

Mara zote ishi maisha yako, kwa sababu muda unavyokwenda mbele, haurudi tena nyuma.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize kama unaishi au unajiandaa kuishi.
Je kuna kitu chochote unachokisubirisha kwenye maisha yako kwa kujiambia utaanza kukifanya baada ya kupata au kuvuka hali fulani?
Kama ndiyo basi jua unakuwa umechagua kuyapoteza maisha yako, maana hayakusubiri.
Utakuja kushtuka siku moja maisha yamefika ukingoni wakati bado hujaanza kuyaishi.

Tafakari;
Maisha ndiyo haya haya, usijidanganye kwamba kuna wakati maisha yatabadilika ndiyo uweze kuyaishi kikamilifu.
Changamoto zitaendelea kuwepo hivyo unachopaswa kufanya ni kuendelea kuyaishi maisha yako kikamilifu bila ya kuahirisha chochote.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorlHardAndYouWillSucceed