2763; Hakuna anayekuangusha.
Ni rahisi sana kulaumu wengine kwamba wanakuangusha au kukukwamisha.
Lakini nataka nikuhakikishie kitu kimoja, hakuna yeyote anayekukwamisha au kukuangusha.
Bali hayo yote unajifanyia wewe mwenyewe.
Kama hujapata au kufika kule unakotaka kufika, hakuna mwingine yeyote ambaye anakuzuia isipokuwa wewe mwenyewe.
Siyo wazazi, mwenza, serikali, uchumi au mazingira vinakuzuia.
Kwa sababu, kwa hali yoyote uliyonayo, kuna wengine ambao wamepitia magumu zaidi yako, lakini wakaweza kupata walichotaka.
Ni kwa sababu walijua hakuna kinachoweza kuwazuia ila wao wenyewe.
Waliamua kuacha kuwategemea au kuwalalamikia wengine.
Wakaamua kuchukua wajibu wa maisha yao wao wenyewe.
Na hilo likawanufaisha sana.
Huenda unajiambia ndiyo, lakini…
Nikuhakikishie tu, lakini yoyote unayojipa ni kujifurahisha tu, haina mashiko yoyote.
Utajiambia lakini watu wamekuibia au kukutapeli.
Na mimi nitakuambia ni wewe ulichagua kuwaamini watu hao bila ya kujisumbua kuwajua kwa undani na kwa hakika.
Utajiambia lakini uchumi ni mgumu na mengine ya aina hiyo.
Na mimi nitakuambia kwenye huo huo uchumi mgumu kuna wengine wengi ambao wanafanya vizuri tu.
Ambacho kitakusaidia sana kwenye maisha yako ni kuweka sababu zote pembeni na kuchukua hatua sahihi.
Kujua hakuna chochote kinachokuzuia au kukuangusha isipokuwa wewe mwenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Nani au nini umekuwa unaona ndiyo kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa unayoyataka?
Jitangazie leo hakuna yeyote anayekukwamisha au kukuangusha bali wewe mwenyewe.
Simama mbele ya kioo na utamwona wazi anayekukwamisha.
Mkabili huyo na hakuna chochote kitakachoweza kukukwamisha kwa namna yoyote ile.
Tafakari;
Mara zote kwenye maisha yako umekuwa unapata chochote unachokitaka sana na ambacho hukubali kukikosa.
Hivyo kama hautakuwa tayari kuyakosa mafanikio, hakuna kitakachokuwa na nguvu ya kukuzuia kuyapata.
Jiwashe moto, ili chochote kitakachojaribu kukuzuia ukiunguze kabisa.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed