2769; Mtego wa mafanikio.

Watu wengi huwa wanashangazwa na hili; kuna watu wanaanzia chini kabisa, wanapambana kweli kweli na kuyapata mafanikio makubwa, kisha wanaanguka.

Hilo limekuwa linaonekana kwa wengi wanaoanzia chini, kupanda juu, kisha kushuka tena chini.

Hali hiyo imekuwa ikisababishwa na mtego wa mafanikio ambao wengi wamekuwa hawauelewi.

Mtego huo wa mafanikio huwa una hatua nne;

Hatua ya kwanza ni kulijua kusudi ambalo linamsukuma mtu kuweka juhudi kubwa na kufanikiwa.

Hatua ya pili ni mafanikio anayoyapata mtu yanamletea umaarufu, anajulikana na wengi na kupata fursa nyingi zaidi.

Hatua ya tatu ni mtu kuzidiwa na fursa. Anashindwa kusema hapana kwa kila fursa inayomjia, jambo linalopelekea kukubali mambo mengi kuliko anavyoweza kuyafanyia kazi.

Hatua ya nne ni anguko, linalotokana na usumbufu ambao unakuwa umetawanya sana nguvu na umakini wa mtu, anaacha kufanya kile ambacho ndiyo kilimpa mafanikio kwa mara ya kwanza na hilo linaleta anguko.

Watu wengi wanaofanikiwa wamekuwa wakinasa kwenye huo mtego kitu ambacho kinapelekea wapate anguko kubwa.

Hatua ya kuchukua;
Jua upo kwenye hatua ipi ya mafanikio kwa sasa na unajizuiaje usiingie kwenye mtego utakaokupeleka kwenye anguko.
Njia pekee ya kufanya hivyo ni kuchagua uwanja wako utakaoendelea kuucheza hata unapokuwa umefanikiwa na kusema hapana kwa fursa, hata kama ni nzuri kiasi gani, kama hazipo kwenye uwanja uliochagua.

Tafakari;
Baada ya kufanikiwa usisahau kile ambacho kimechangia kuyajenga mafanikio yako. Lazima uendelee kukifanya kwa ubora zaidi ili uweze kudumu kwenye mafanikio uliyopata.
La sivyo utapata anguko kubwa kwenye kila mafanikio unayokuwa umeyapata.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed