2770; Lazima uwaamini watu.
Jamii zote zimejengwa kwenye msingi wa kuaminiana.
Ni pale watu wanapoaminiana ndiyo jamii inakuwa imara na watu kufanikiwa.
Na pale imani baina ya watu inapokosekana, jamii inakuwa dhaifu na watu kushindwa.
Ni imani kwa wengine kwamba wanajua wanachofanya na wana nia njema ndiyo inafanya kila jamii kuweza kwenda vizuri.
Huwa tunafanya mambo mengi kwa imani tu, kwa sababu hatuna namna ya kujithibitishia kila kitu sisi wenyewe.
Unapokwenda kwenye hoteli au mgahawa kupata chakula, huna njia ya kukuthibitishia kwamba kila kitu kimefanyika kwa usahihi. Unaamini tu hivyo na hilo ndiyo linakuwezesha kula chakula.
Unapokuwa barabarani huna njia ya kuthibitisha kama madereva wote ni sahihi, wana elimu ya udereva na utulivu wa akili. Unaamini tu hivyo na hilo ndiyo linakuwezesha kutumia barabara.
Hiyo ni mifano michache, lakini ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha yetu.
Kwa mambo yote ambayo tunashirikiana na wengine, kwa sehemu kubwa tunafanya kwa imani kwa sababu hatuna njia ya kujithibitishia wenyewe kila kitu.
Kuna mambo makubwa mawili ya kujifunza hapa;
Jambo la kwanza ni KUAMINI.
Ni lazima uweze kuwaamini wengine ili uweze kushirikiana nao.
Kujiambia kwamba watu hawaaminiki au huwezi kumwamini yeyote ni kujiwekea wakati mgumu kupata watu wa kushirikiana nao.
Ndiyo kuna ambao utawaamini na wasiwe sahihi, lakini hilo lisikukatishe tamaa.
Hiyo haiondoi umuhimu wa kuthibitisha mambo pale inapowezekana kufanya hivyo.
Muhimu ni usijikwamishe kwa sababu ya kushindwa kuwaamini wengine. Waamini watu hata kama wanaweza kukuumiza, hilo litakupa nafasi ya kupiga hatua zaidi.
Jambo la pili ni KUAMINIKA.
Cheza vizuri nafasi yako kwenye jamii.
Aminika kwenye kile unachoiahidi jamii.
Unaposema unafanya kitu, kifanye kweli.
Ahidi na timiza.
Kuwa bora kwenye kile unachokifanya.
Warahisishie watu kuweza kukutegemea kwenye kile unachofanya na unachowaahidi.
Kadiri unavyoaminika na wengine, ndivyo unavyokuwa kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa.
Hatua ya kuchukua;
Amini wengine na wape watu sababu ya kukuamini.
Kama mtu hajakupa sababu ya kutokumwamini basi endelea kumwamini.
Na mtu mmoja kuvunja imani uliyoweka kwake haimaanishi wengine hawaaminiki.
Endelea kuwaamini watu hata kama hilo linakuweka kwenye hatari.
Maana ndiyo njia pekee ya kuweza kupiga hatua.
Tafakari;
Kujiambia huwezi kumwamini yeyote au watu hawaaminiki ni kujizuia usifanikiwe.
Kuna mengi ambayo huwezi kuthibitisha wewe mwenyewe.
Kuamini wengine ni hitaji muhimu sana kwenye mafanikio yako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed
Asante nitawaamini watu na Mimi nitajiaminisha kwa kile nilicho ahidi na kutimiza
LikeLike