#SheriaYaLeo (274/366); Usiende zaidi ya lengo.
Kiini cha mkakati ni kudhibiti kile kinachofuata baada ya kufikia lengo.
Maana ushindi huwa una hatari ya kuvuruga kile kinachofuata kwa njia mbili.
Moja ni kutaka kurudia kufanya yale uliyofanya ukidhani yatakupa matokeo uliyopata. Unajikuta ukijenga mazoea bila hata kuangalia kama ni mazoea sahihi kwako.
Mbili ni mafanikio yanakupanda kichwani kwa kuteka hisia zako na kujiona huwezi kushindwa. Hilo linapelekea uchukue hatua za hatari ambazo zinaweza kuharibu ushindi ambao umeshaupata.
Somo hapa ni rahisi; wanaofanikiwa na kuweza kudumu kwenye mafanikio yao huwa wanabadili hatua wanazochukua na kuendana na hali ilivyo. Huwa wanajifunza na kuboresha zaidi kadiri wanavyokwenda.
Badala ya kuruhusu ushindi wao kuwapeleka tu mbele, huwa wanarudi nyuma ili kuweza kuona kule wanakokwenda.
Ndani yao wanakuwa na kinga ya kuzuia ushindi waliopata usiwe sumu kwao.
Hilo linawawezesha kuwa na udhibiti kwenye hisia zao na kuweza kufanya maamuzi sahihi na bora.
Hawaruhusu ushindi wao kuwa sumu kwao kwa sababu wanajua kuna mchango wa bahati kwenye ushindi waliopata.
Kama wanavyosema kwenye shule ya kuendesha farasi, unapaswa kuweza kujidhibiti wewe mwenyewe kwanza kabla hujaweza kumdhibiti farasi.
Kama hutaweza kujidhibiti mwenyewe, mafanikio yatakupoteza kabisa.
Sheria ya leo; Wakati wa ushindi ndiyo wakati wenye hatari kubwa sana ya kuanguka. Usiruhusu mafanikio yakupande kichwani. Hakuna mbadala wa mikakati na mipango sahihi. Jiwekee lengo na ukishalifikia usiendelee zaidi ya hapo kabla kwanza hujajifanyia tathmini.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji