2775; Ushauri ni ule ule.
Kwenye kitabu cha The Richest Man In Babilon, watu wawili ambao licha ya kuweka juhudi kubwa kwenye kazi bado wapo kwenye umasikini mkubwa, waliamua kwenda kuomba ushauri kwa rafiki yao wa utotoni ambaye alikuwa na utajiri mkubwa.
Baada ya kuwasikiliza, mtu huyo tajiri aliwashirikisha hadithi ya jinsi alivyopata ushauri ambao ndiyo ulimwezesha kujenga utajiri mkubwa.
Msingi wa ushauri huo ulikuwa ni kujilipa wewe mwenyewe kwanza kwenye kila kipato unachoingiza, kisha kuwekeza hicho unachojilipa kwenye maeneo ambayo yanazalisha faida zaidi.
Baada ya kusikia ushauri huo, watu hao wawili walimuuliza tena mtu huyo tajiri ni hatua gani ambazo wao wanaweza kuchukua, hasa ukizingatia kwamba umri umekwenda.
Ni kama walidhani kwa kuwa umri wao umekwenda basi wanahitaji ushauri wa tofauti.
Lakini mtu yule tajiri aliwajibu ushauri ni ule ule, wataweza kujenga utajiri kama watajilipa wao wenyewe kwanza na kuwekeza kile wanachojilipa.
Kuna somo kubwa sana hapo rafiki yangu. Kuna wakati huo tunaona kwa hali zetu tunazodhani ni za tofauti, ushauri au kanuni wanazotumia wengine sisi hazitufai.
Lakini ukweli ni kwamba ushauri na kanuni ni zile zile.
Haijalishi kama tumewahi au kuchelewa kusikia.
Kama tunataka kupiga hatua kutoka pale tulipo, tunapaswa kufuata njia sahihi ambayo walioweza kupiga hatua waliitumia pia.
Hatua ya kuchukua;
Ni rahisi kuona hali yako ni ya tofauti hivyo ushauri uliowasaidia wengine kwako hauwezi kufanya kazi.
Hilo siyo sahihi, ushauri ambao unatokana na misingi na kanuni sahihi unafanya kazi kwa kila mtu.
Acha kujidanganya kwamba hali yako ni ya tofauti au ya kipekee sana.
Fanyia kazi ushauri sahihi na utaweza kupiga hatua kubwa.
Tafakari;
Ubishi ni moja ya vitu ambavyo vimekuwa kikwazo cha mafanikio kwa walio wengi.
Kitu kimefanya kazi kwa wengine, lakini kwako unataka kuleta ubishi kwamba hakiwezi kufanya kazi.
Kila unapojikuta unaleta ubishi kwenye ushauri unaopewa, jiulize kwa nini anayekupa ushauri huo amefanikiwa kuliko wewe.
Na hapo utagundua ni kwa sababu hakuwa mbishi kama wewe.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed
asante
LikeLike