2776; Wewe na hayo mawazo yako ya kukwepa kazi.
Tangu kuwepo kwa dunia, kumekuwa na njia moja tu ya mtu kupata kile anachotaka.
Njia hiyo ni KAZI.
Lakini mara kwa mara huwa zinakuja hadaa za namna ya kuweza kupata unachotaka bila ya kuweka kazi.
Kwa kuwa wengi hawapendi kazi, huwa wanakimbizana na njia hizo zinazoonekana ni mpya na bora.
Lakini mwisho wa siku wanajikuta wamepoteza muda na fedha zao, huku wakiwa hakuna walichopata.
Watu wote wenye mafanikio makubwa na ambao pia ni matajiri wakubwa duniani, wamekuwa wanafanya kazi sana.
Halafu unaamini wewe unaweza kuwa mjanja kuliko wao, kwa kukutana na njia ya kipekee ya kukupa mafanikio na utajiri bila ya kuweka kazi!
Jifikirie mara mbili rafiki.
Unadhani kama kungekuwa na njia ya mkato ya kufanikiwa ingebaki kuwa ya mkato?
Unadhani ni siri ambayo dunia nzima itakuwa imefichwa na wewe ndiye mwenye bahati ya kuijua?
Rafiki, yeyote anayekuja kwako akiwa na siri ya kufanikiwa na kupata utajiri, siri yake kuu ni moja, anakutapeli na kukulaghai wewe ili apate anachotaka.
Hakuna anachojali kuhusu wewe na wala hakuna unachokwenda kupata.
Anachofanya ni kuteka hisia zako na kukuhadaa.
Kwenye haya maisha, ukiweka imani yako kwenye kazi, unayarahisisha sana.
Japo wengi hudhani maisha yanakuwa magumu kwa sababu ya kazi, ukweli ni kwa kuamini kwenye kazi maisha yanakuwa rahisi.
Angalia, hakuna anayeweza kukuhadaa na kukutapeli kama unaamini kwenye kazi.
Watu wote wanaohadaiwa na kutapeliwa, chanzo ni kuamini kuna siri ya mafanikio ambayo haihusishi kazi.
Lakini pia muda na nguvu unazotumia kuhangaika na njia za mkato zisizo na tija ukipeleka hivyo hivyo kwenye kazi utapata matokeo mazuri na ya uhakika zaidi.
Utakuwa pazuri zaidi kwa kuamini kwenye kazi na kuacha kuhangaika na mambo yasiyo na tija.
Kila unapopata mawazo ya kukwepa kazi, au watu wanapokuja kwako wakijinasibu kuwa na siri ya kupata mafanikio bila kazi, jikumbushe kazi ndiyo msingi mkuu na usitetereke kwenye hilo.
Usihangaike kabisa na hayo unayoambiwa hayahitaji kazi.
Jua wazi kama kitu hakihitaji kazi, basi wewe ndiyo kazi yenyewe.
Kuna usemi kwamba kama haupo kwenye meza ya chakula, basi wewe ndiye chakula chenyewe.
Kadhalika kwenye kazi, kama unaambiwa kuna njia ya kufanikiwa bila kuweka kazi, basi jua wewe ndiyo kazi yenyewe na mafanikio hayatakuwa yako bali ya wengine.
Hatua ya kuchukua;
Pima kila kitu kwa kazi unayopaswa kuweka ili kupata matokeo.
Kama unaambiwa kitu hakihitaji uweke kazi ila utapata matokeo, kimbia haraka, wanataka kukugeuza wewe kuwa kazi yao.
Tafakari;
Kama kungekuwa na njia ya kweli ya kufanikiwa isiyohusisha kazi, isingekuwa siri iliyofichwa kiasi cha wewe kuwa mmoja wa wachache wanaoijua. Ingekuwa ndiyo njia kuu ya mafanikio inayotumiwa na kila mtu.
Hivyo epuka sana siri unazopewa ambazo zinahidi mafanikio bila kazi. Siri pekee ambayo huambiwi ni wewe kugeuzwa kuwa fursa kwa wengine.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed