2778; Itafanyika njia kwa ajili yako.
Ukweli mmoja ambao watu wengi wamekuwa hawaelewi kwenye maisha ni huu, kila mtu huwa anapata kile anachokitaka kweli kwenye maisha yake.
Yaani kama kuna kitu ambacho unakitaka sana kwenye maisha yako, na hakuna namna unakubali kutokukipata, basi unakipata.
Hata pale inapoonekana hakuna njia kabisa, unapokuwa king’ang’anizi kwenye kile unachotaka, basi njia hutengenezwa kwa ajili yako.
Sijui umeelewa vizuri hapo rafiki yangu.
Yaani kama kuna kitu hujakipata kwenye maisha yako, tatizo siyo kwamba hakuna njia ya kukipata.
Bali tatizo ni kwamba hujakitaka hasa.
Unapokitaka kitu kweli, unapokuwa huna mbadala mwingine, milango hufunguka.
Upo usemi kwamba dunia huwa inasalimu amri kwa yeyote anayekataa kushindwa.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa wewe.
Iambie dunia ni nini unataka na kataa kabisa kushindwa.
Ng’ang’ana na kile unachotaka mpaka ukipate.
Usiwe na mbadala mwingine kwenye hilo.
Ifanye dunia ijue wazi hicho ndiyo unachotaka na haupo tayari kukubali kingine chochote chini ya hapo.
Hata kama inaonekana wazi kwamba hakuna njia, dunia itakuwa tayari kutengeneza njia kwa ajili yako.
Maendeleo yote ambayo yamepatikana hapa duniani, yaliletwa na watu waliokuwa ving’ang’anizi kwenye kile walichotaka.
Walipingwa, walikosolewa, walibezwa na kuchekwa.
Lakini hawakujali yote hayo, badala yake walisimamia kile walichotaka.
Mwisho dunia iliwapa njia na kila mtu akanufaika kwa hilo.
Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani kikubwa kimoja ambacho unakitaka sana kwenye maisha yako na haupo tayari kukikosa? Kiweke wazi na kisimamie kwa kila namna bila ya kutetereka.
Dunia itakukatalia mwanzoni, lakini ung’ang’anizi wako utaifanya dunia itengeneze njia kwa ajili yako.
Tafakari;
Dunia huwa kwanza inawapima watu kabla haijawapa kile wanachotaka. Kwanza inawanyima ili kuona wamejitoa kiasi gani kukipata. Halafu baadaye inawapa kidogo kuona kama watalewa kile kidogo walichopata. Ni pale mtu anapovuka vikwazo hivyo viwili ndiyo dunia inamwona kweli amejitoa kupata anachotaka na hapo inampatia.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed