#SheriaYaLeo (282/366); Wazimu wa kundi.
Wewe peke yako, ukiwa na wazo au mpango ambao ni wa kijinga, watu watakutahadharisha mara moja na kukurudisha kwenye uhalisia.
Lakini hilo linapokuwa kwenye kundi, kinyume chake hutokea. Hata kama wazo au mpango ni wa kijinga kiasi gani, kama umekubalika na kundi, kila mtu anakubaliana nao bila kuhoji usahihi wake.
Kama Friedrich Nietzsche alivyowahi kusema, wazimu ni adimu kwa mtu mmoja mmoja, lakini kwenye makundi ya watu ni kitu cha kawaida.
Kila unapoona ukikubaliana na wazo au mpango kwa sababu kundi zima linakubaliana nayo, ni vyema kujiweka pembeni na kuangalia kwa mantiki.
Mara nyingi ndani ya kundi unasombwa na hisia wanazokuwa nazo wengine na kujikuta unakubaliana na vitu ambavyo peke yako usingekubaliana navyo.
Mara kwa mara kaa nje ya kundi ili uweze kuangalia uhalisia kwa kutumia mantiki badala tu ya kutekwa na hisia zilizopo kwenye kundi.
Sheria ya leo; Kamwe usikubali kupoteza uwezo wako wa kushuku, kudadisi na kutafakari mambo kwa mantiki na peke yako. Kutekwa na kulitegemea kundi ni kukubali kuhadaiwa na maamuzi ambayo siyo sahihi ila yameteka hisia. Ni rahisi kuuona na kuuvuka wazimu wa kundi pale unapoweza kutoka nje ya kundi hilo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji