2779; Kutokutaka kupitwa.

Habari, tv, umbeya, udaku, majungu na mitandao ya kijamii ni vitu ambavyo vimekuwa na nguvu kubwa kwa wengi kwa sababu vinatumia msingi mmoja muhimu; hofu ya kupitwa.

Kwa Kiingereza wanaita FOMO (Fear Of Missing Out).
Hebu fikiria, kila siku kuna habari mpasuko (breaking news). Unadhani zote hizo ni habari muhimu? La hasha, kila habari itafanywa kuonekana ni muhimu ili watu wasitake kuikosa.

Angalia tamthilia yoyote yenye mwendelezo, huwa wanaikatishia pale patamu. Pale ambapo utakuwa unajiuliza nini kitaendelea? Ili uhakikishe unaangalia sehemu inayofuata.

Umbeya, udaku na majungu vyote vipo kundi moja. Vinakufanya uone kuna vitu muhimu utajua kuhusu watu, ambavyo hupaswi kukubali vikupite.

Tukienda kwenye mitandao ya kijamii, hiyo ndiyo baba lao, yaani hiyo imeweza kutumia hofu hiyo ya kupitwa kuwanasa watu kwenye mitandao hiyo mpaka wamekuwa na uraibu.
Kila unapotembelea mitandao hiyo, hutaki kutoka, unataka uendelee kuperuzi tu kuona vitu zaidi.
Kila unapotaka kutoka unaona kitu kingine ambacho unadhani hakipaswi kukupita.
Ulipanga kuperuzi kwa dakika tano, unajikuta nusu saa imepita bado unaperuzi tu.

Rafiki, kutokutaka kupitwa ni kitu ambacho tumekirithi kwa watangulizi wetu.
Ambao waliishi kwenye mazingira hatari na hivyo walipaswa kufuatilia kila kitu ili kuweza kuendelea kuwa hai.

Lakini kwa sasa hatupo tena kwenye mazingira ya aina hiyo, lakini bado hofu hiyo ipo ndani yetu na wajanja wachache wanaitumia kwa manufaa yao.

Unachopaswa kujua ni hiki, kadiri ambavyo hutaki kupitwa na mengi yanayoendelea ndivyo unavyopitwa na mafanikio yako mwenyewe.
Yaani kadiri unavyohangaika na mambo ya wengine, ndivyo unavyojichelewesha kufanikiwa.

Kama unahangaika na kila ambacho kinakuja kwako kama vile ni muhimu sana, hutabaki na muda wala nguvu za kufanya yale yaliyo muhimu kwako ili kufanikiwa.

Ili ufanikiwe, lazima uwe na vipaumbele sahihi. Lazima ujali mambo yako zaidi ya unavyojali mambo ya wengine ambayo huwezi kuyaathiri moja kwa moja.

Unapaswa kuachana na hofu ya kupitwa na kufurahia kupitwa. Yaani ufurahie kupitwa na mengi yanayoendelea, ili uhangaike na yake muhimu zaidi kwako.

Kwa Kiingereza wanaita JOMO (Joy Of Missing Out). Lazima ufurahie kupitwa na yale yasiyo na tija, ili upeleke muda na nguvu zako kwenye yale muhimu zaidi kwako.

Dunia haitasimama kwa sababu wewe umeacha kujali yale yasiyokuwa na tija kwako.
Badala yake itaendelea kwenda kama inavyoenda, huku wewe ukiwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.

Hatua ya kuchukua;
Acha mara moja kuendeshwa na FOMO na anza kuendeshwa na JOMO.
Orodhesha mambo yote ambayo ulikuwa unahofia yatakupita kisha furahia kupitwa nayo.
Kisha orodhesha yale muhimu kwa mafanikio yako, yale ambayo kwa kuyapa kipaumbele kikubwa utaweza kupata mafanikio unayoyataka.

Tafakari;
Ukifa leo, dunia haitasimama hata kwa sekunde moja, kila kitu kitaendelea kama kawaida, kama vile hujawahi kuwepo kabisa. Hivyo acha kujipa umuhimu usio sahihi, acha kuhangaika na yale unayodhani hayapaswi kukupita. Weka vipaumbele vyako sahihi, ili uweze kufanya kitu kimachoacha alama hapa duniani hata ukiondoka leo.
Hakuna mtu amewahi kuacha alama hapa duniani kwa kufuatilia habari zote, kujua mambo ya wengine, kuangalia kila tamthilia na kufuatilia kila kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii.
Weka vipaumbele vyako kwa usahihi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed