2780; Siyo muda, ni vipaumbele.
Watu huwa wanapenda sana kutumia sababu ya ‘sina muda’ kama kikwazo kwao katika kuchukua hatua ili kufanikiwa.
Lakini hiyo ni sababu ya uongo na isiyo na ushahidi wa uhakika.
Iko hivi, watu wote tuna muda sawa na unaolingana. Wote tuna masaa 24 tu kwa siku, hakuna awezaye kujiongezea hata sekunde moja.
Hivyo ukweli ni watu wote tuna muda.
Tofauti inakuja kwenye matumizi ya muda huo, au kwa maneno mengine ni vipaumbele ambavyo watu wanakuwa navyo.
Vitu vyote unavyopata muda wa kuvifanya ndiyo umevipa kupaumbele cha juu. Yaani hivyo ndiyo vitu ambavyo kwako ni muhimu zaidi.
Hivyo kama mafanikio yako ni kitu muhimu kwako, basi lazima utatenga muda wa kufanya yale unayopaswa kuyafanya ili ufanikiwe.
Kuna muda mwingi sana ambao kila mtu huwa anaupoteza kwa kuhangaika kufanya mambo yasiyokuwa na tija kwetu.
Fikiria muda wote ambao umekuwa unautumia kufuatilia maisha ya wengine, kuperuzi mitandao ya kijamii na kuhangaika na habari mbalimbali.
Kama ungeokoa muda huo na kuupeleka kwenye kile unachotaka kufanikiwa, ndani ya miaka 5 ungekuwa umepiga hatua kubwa mno.
Uzuri ni bado hujachelewa, unaweza kuanza sasa kuwa na vipaumbele sahihi kwa kuacha kupoteza muda wako kwenye mambo yasiyokuwa na tija.
Hatua ya kuchukua;
Jifanyie ukaguzi kwenye matumizi yako ya muda.
Chukua karatasi na uigawe pande mbili.
Upande wa kwanza orodhesha mambo yote uliyofanya kwenye wiki moja iliyopita.
Upande wa pili orodhesha malengo uliyonayo.
Kisha uoanisha ulichofanya na lengo ambalo kitu hicho kinasaidia kufikia.
Kwa yale ambayo ulifanya ila hayachangii kwenye lengo lolote, acha kuyafanya mara moja.
Yaani jiambie hufayafanya tena na simamia hilo.
Utajikuta ukiwa na muda wa kutosha kufanyia kazi mafanikio yako.
Tafakari;
Kila mtu ana muda sawa, tunatofautiana kwenye namna tunavyotumia muda huo.
Kila unapojiambia huna muda, jikamate na ujiulize ni mambo gani umeyapa kipaumbele kisichokuwa sahihi.
Hapo utajionea mwenyewe jinsi umekuwa ukipoteza muda wako kwa mambo yasiyokuwa na tija.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed