#SheriaYaLeo (285/366); Jihadhari na wivu.

Katika hisia zote za binadamu, hakuna ambayo ni mbaya na yenye madhara kama wivu.
Hisia kwamba wengine wametuzidi kwenye yale ambayo tunayataka sana kama mali, umaarufu na mamlaka.

Huwa tunaona tunastahili kupata kwa wingi kama hao wengine, lakini tatizo linakuja kwamba tunakuwa hatuna namna ya kupata kile tunachotaka.

Wivu huwa ni kukiri kwamba tupo chini ya wengine kwa sababu ya wao kutuzidi kwenye kile walichonacho.
Hilo linaumiza zaidi pale wengine wanapojua kwamba tunajiona wa chini.

Kuepuka hilo, wengi wamekuwa wanaficha hisia za wivu pale zinapoibuka ndani yao.
Wanachofanya ni kuficha hisia hizo za wivu nyuma ya mambo kama kukosekana kwa usawa na hali ya upendeleo.
Wanaona kwamba wale waliowazidi kuna namna wamependelewa hivyo kupata zaidi.

Japo kwa nje linaweza kuchukuliwa hivyo, ndani ya mtu bado hali hiyo inaendelea kumuumiza na kumfanya ajisikie vibaya na wa chini.
Hilo hutengeneza hasira ndani ya mtu na kumsukuma kufanya kitu cha kumdhuru yule anayemwonea wivu.

Ubaya wa hisia za wivu ni kwamba huwa hazina mwisho. Kwani hata baada ya kumdhuru anayemwonea wivu, bado ataona wengine ambao wamemzidi.
Kila wakati kunakuwa na watu na vitu vya kuonea wivu.

Sheria ya leo; Wivu ndiyo hisia mbaya kuliko zote kwa binadamu. Unapaswa kuiharibu kabla haijakuharibu wewe. Tengeneza hali ya kujiamini na kujikubali, tumia viwango vyako vya ndani kujipima na acha kujilinganisha na wengine au vingine vya nje.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji