#SheriaYaLeo (286/366); Ona vitu kama vilivyo na siyo kama hisia zako zinavyokusukuma.
Unapaswa kujua pale unaposukumwa na hisia katika maamuzi na kujidhibiti ili usilete madhara.
Hiyo ni kwa sababu hisia huwa zinatuzuia tusione vitu kama vilivyo.
Hofu inakufanya umkuze zaidi adui na kukimbilia kujihami haraka.
Hasira zinakufanya ukimbilie kuchukua hatua kitu kitakachokuondolea machaguo mengine mazuri kwako.
Kujiamini kupitiliza, hasa baada ya kupata mafanikio, kutapelekea uende zaidi ya mipango yako.
Upendo huwa unakupofusha usione mbinu chafu za wale walio upande wako.
Kila hisia ina nguvu ya kukuzuia usiuone uhalisia, badala yake uone kile unachotaka kuona.
Dawa pekee ya hili ni kutambua kwamba hutaweza kuondokana na hisia kabisa, hivyo kutambua pale zinapokuwa zinakutawala na kuzuia zisiathiri maamuzi yako.
Unapokuwa na mafanikio, ongeza tahadhari.
Unapokuwa na hasira, usifanye chochote.
Unapokuwa na hofu, jua utakuza mambo kuliko uhalisia wake.
Kujua madhara ya hisia unazokuwa nazo kabla hazijakutawala inakusaidia kujizuia usitawaliwe na hisia hizo na kufanya maamuzi yasiyo na tija.
Sheria ya leo; Maisha yanatutaka tuwe na uhalisia wa hali ya juu kabisa, kuona vitu jinsi vilivyo na siyo tunavyotaka kuviona sisi. Kadiri unavyoweza kudhibiti hisia zako zisiathiri maamuzi, ndivyo unavyoweza kwenda kwenye uhalisia huo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji