2784; Tatizo ni kujidanganya.

Mwanafizikia Richard Feynman aliwahi kunukuliwa akisema jukumu lako la kwanza kwenye maisha ni kutokujidanganya wewe mwenyewe. Na hakuna mtu rahisi kumdanganya kama wewe mwenyewe.

Kauli hiyo ina ukweli mkubwa sana ambao ukiuelewa na kuufanyia kazi hakuna kitu kitakachokushinda kwenye maisha yako.

Kitu cha kwanza kabisa unachopaswa kuacha kujidanganya mara moja ni kuhusu mafanikio.
Kama bado hujafanikiwa, kama hujapata kile hasa unachotaka kwenye maisha yako, ni kwa sababu hujakitaka kweli.

Ndiyo, hujakitaka kweli kweli na kuwa tayari kufanya kila unachopaswa ili kukipata.
Sasa kwa kuwa hupendi kujiambia ukweli, unatafuta njia ya kujidanganya ambayo ndiyo imekuweka hapo ulipo sasa.

Unajiambia huna muda, wakati masaa yako kwa siku ni 24 kama waliyonayo wengine na unayatumia yote bila kubakiza hata chenchi.
Sehemu kubwa ya muda huo unatumia kwa mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Lakini kwa kuwa unajidanganya, hulioni hilo. Unaendelea kuimba huna muda.

Unajiambia huna fedha, wakati maisha yako yanaendelea. Yale mahitaji ya msingi uliyonayo, unahakikisha unayapata kwa namna yoyote ile. Hata uwe huna fedha kiasi gani, hutakaa na njaa kwa muda mrefu, hutatembea uchi, hutakosa mawasiliano.
Kwa namna fulani unahakikisha maisha yako yanaendelea, lakini zaidi ya hapo unarudi kwenye kujidanganya kwako.

Unajionea mwenyewe rafiki yangu, sababu ya kwanza kwako kutokupata kile unachotaka ni kujidanganya.
Umejiridhisha na pale ulipo sasa, lakini kwa kuwa hutaki kukubali hilo, umetafuta sababu ya uongo ya kukufanya ujisikie vizuri.

Wajibu wangu mimi kama Kocha wako ni kuhakikisha hujisikii vizuri kuendelea kuwa hapo ulipo.
Ni kuuweka wazi uongo ambao umekuwa unautumia kama kivuli cha kujificha.
Ni kukuambia wazi bila ya kupepesa macho kwamba wewe mwenyewe ndiye unayejizuia kufanikiwa.

Labda nikupe mfano mmoja ambao utaendelea kuutafakari na kuona namna gani kujidanganya kumeyagharimu maisha yako.

Nikikupa namba za simu za watu 100 nikakuhakikoshia kwamba hao watu wapo tayari kununua unachouza, wanachosubiri ni wewe tu uwapigie simu. Je utakosa muda wa kuwapigia na kuja na sababu mbalimbali kwa nini huwezi kuwapigia?

Vipi nikikupa watu wengine 10 ambao tayari wanazo fedha, wanakusubiri tu uwafuate kwenda kuzichukua. Je utajiambia huna muda au huwezi kwenda kuwafuata?

Sasa turudi kwenye ukweli, ni fedha kiasi gani umeshindwa kuzikusanya kwa kushindwa kuwasiliana na kuwatembelea wateja wako?
Na huo muda ambao hukufanya hivyo, unaweza kutuonyesha ni lipi la maana uliutumia kufanya?

Kila unaposhindwa kufanya au kupata unachotaka, swali la kwanza unalopaswa kujiuliza ni hili; wapi ninapojidanganya?
Bila ya kuwa muwazi kwako mwenyewe, bila ya kujichunguza na kujibana wewe mwenyewe kwa uhakika, mafanikio makubwa yatakuwa magumu sana kwako.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku anza kwa kuorodhesha yale ambayo umekuwa unajidanganya na yanakupa faraja hewa inayokuzuia kufanikiwa. Kisha jipe ukweli kwenye kila eneo na ishi ukweli huo.
Kama umekuwa unajiambia huna muda, kubali huko ni kujidanganya. Jiambie muda unao, kisha angalia namna gani bora kwako kutumia masaa 24 ya siku unayokuwa nayo.
Hivyo pia kwenye fedha, watu, mawazo mazuri n.k.
Vunja kujidanganya ambako umekuwa unafanya na dhihirisha ukweli kwako ili uweze kufanikiwa.

Tafakari;
Upo hapo ulipo sasa, kutokana na yale ambayo umekuwa unafanya huko nyuma. Sehemu kubwa ya yaliyokufikisha hapo ulipo ni kujidanganya.
Kuendelea vile ulivyokuwa huko nyuma, utaendelea kupata matokeo unayopata sasa.
Kama unataka kupata matokeo tofauti na unayopata sasa, lazima uwe mtu wa tofauti na ulivyokuwa huko nyuma.
Na tofauti pekee unayoihitaji ni kuacha kujidanganya.
Anza kufanyia kazi hilo leo na utaanza kuyaona mabadiliko.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed