2788; Usiage mashindano.

Fikiria timu yako unayoipenda ya mpira wa miguu.

Imeingia uwanjani kushindana na timu nyingine.

Dakika tano tu za kwanza za mchezo, timu yako inafungwa goli moja.

Cha kushangaza sasa, baada ya kufungwa goli hilo moja, wachezaji wote wanaamu kuondoka uwanjani.
Wanajiona hawafai kabisa, wamefungwa haraka na hawana sababu ya kuendelea tena.

Je unaweza kuwaelewa wachezaji hao?
Yaani wanakata tamaa dakika ya 5 wakati mchezo una dakika 90? Na tena wakati mwingine kuna mpaka dakika za ziada!

Utawashangaa wachezaji kwenye hilo, wakati wewe mwenyewe ndiyo umekuwa unaishi hivyo kwa uhalisia.

Ni mambo mangapi umeacha kufanya kwenye maisha yako kwa sababu tu matokeo ya mwanzo hayakuwa mazuri?

Kuwa tu mkweli kwako na pitia mipango yote mikubwa ambayo umewahi kujiwekea kwenye maisha yako.
Angalia uliitekeleza kwa muda gani kabla hujaacha kuyafanya.

Hapo utagundua kwamba umekuwa unayakimbia mambo mapema pale tu unapopata matokeo tofauti na ulivyotegemea.

Ulipanga uwe unaamka asubuhi na mapema, siku za mwanzo unafanya hivyo. Siku moja unachelewa kuamka mapema na hapo ndiyo ukawa mwisho wa kuamka mapema, unajiona huwezi tena.

Ulipanga kupiga simu na kuwatembelea wateja wa biashara yako. Unaanza ukiwa na shauku kubwa. Lakini wateja unakwasiliana nao na kuwatembelea hawaonyeshi ushirikiano. Wanakataa hata kukupa muda wao.
Unaona ni zoezi lisilofaa na kuachana nalo.

Kuna mengine mengi ambayo umekuwa unayakimbia kwenye maisha yako, kwa sababu tu mwanzoni hujapata matokeo ambayo uliyatarajia.

Rafiki, kama ambavyo mchezo wowote una muda wake wa kuchezwa, hata timu ikianza vibaya kiasi gani, itapaswa kuendelea na mchezo kwa muda wote.
Na katika hicho kipindi kocha anachukua hatua mbalimbali kurekebisha makosa yanayojitokeza ili timu ifanye vizuri.

Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kuwa.
Hupaswi kuyaaga mashindano mapema hata kama ni matokeo gani unayoyapata.
Ukishaingia kwenye mashindano, endelea nayo mpaka mwisho wake.
Unachohitaji kufanya ni kukazana kuwa bora kadiri unavyokwenda.

Kwa chochote unachopanga kufanya, matokeo, hasa ya mwanzo, hayatakuwa kama ulivyopanga.
Wajibu wako ni kuendelea kukaa kwenye mashindano na kukazana kuwa bora zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Kwa yale ambayo umeamua kufanya, amua kwamba utaendelea kuyafanya hata kama hupati matokeo uliyotarajia. Utaendelea kujitathmini na kuboresha zaidi. Lengo ni kuendelea kufanya mpaka pale utakapopata kile unachotaka.

Tafakari;
Hatua ya kwanza muhimu ya kuchukua ili kupata ushindi wa aina yoyote ile ni kuingia kwenye mashindano na kukaa kwenye mashindano hayo bila ya kuyakimbia.
Ukishaingia kwenye mashindano, nenda mpaka mwisho bila ya kuyakimbia.
Mafanikio yanahitaji uvumilivu na ung’ang’anizi kuliko kitu kingine chochote.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed