2790; Kuna anayeweza kununua kwako?

Hivi karibuni nilikutana na ujumbe unaozunguka mtandaoni unaosema kampuni ya magari ya Lamboghini (moja ya magari ya bei ghali zaidi) huwa haijitangazi kwenye tv kwa sababu watu wanaoweza kumudu kununua aina hiyo ya magari, hutawakuta wamekaa wanaangalia tv.

Ujumbe huo unaweza kuchukuliwa kama kichekesho, lakini ndani yake umebeba funzo kubwa sana.
Funzo hilo ni kwamba unapaswa kuwa pale ambapo wateja wako wapo.

Unapaswa kuwafikia vyema wale unaowalenga kwenye kile unachofanya.
Na njia za kuwafikia zinatofautiana kulingana na kile kinachofanyika.

Kwa sababu watu fulani wametumia njia fulani wakafanikiwa, haimaanishi na wewe ukitumia njia hiyo utafanikiwa pia.

Na pia kutaka kumfikia kila mtu ni matumizi mabaya ya rasilimali ulizonazo kwa uhaba.
Hata ukimfikia kila mtu, bado siyo wote watakaonunua.

Hivyo nji bora ni kuwajua wale unaowalenga na kule wanakopatikana kwa wingi kisha kuwa huko kwa muda mrefu.

Epuka sana kukaa eneo ambalo unaowafikia siyo unaowalenga. Itakuwa rahisi kwao kukukatisha wewe tamaa kwa matokeo mabovu unayopata na maneno yao yasiyo sahihi.

Hatua ya kuchukua;
Kama bado hujafikia uhuru wa kifedha, sehemu kubwa sana ya mud wako unapaswa kuutumia kwa wale wenye uwezo wa kununua kwako. Fanya kila unachopaswa ili kufika mbele ya wale unaowalenga na kuweza kuwashawishi.

Tafakari;
Kuna muda na nguvu nyingi unazotapanya hovyo na hivyo kukosa tija kwako.
Sasa kuwa na mkakati sahihi, kuhangaika na yale tu yenye tija.
Muda wako ni mfupi, nguvu zako zina ukomo, usipoteze rasilimali hizo kwa mambo yasiyo na tija.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed