#SheriaYaLeo (296/366); Usipotezwe na vitu visivyo na tija.

Kuna wakati unajikuta umezidiwa na majukumu ambayo unapaswa kuyatekeleza.
Unajikuta ukiwa na mambo mengi ya kufanya, lakini muda wa kuyafanya unakuwa mdogo.

Ni katika wakati huo ndiyo unapata hali ya kuvurugwa, kwa kuona kuna mambo unapoteza au unayakosa kwa sababu umepoteza udhibiti.

Unapojikuta kwenye hali hii, kitu kimoja unachopaswa kujua ni umekosa vipaumbele.
Unakuwa umeruhusu kila kitu kuwa muhimu kwako hata yale ambayo hayana tija.

Unakuwa umesambaza sana muda wako na nguvu zako kiasi kwamba hakuna matokeo yoyote mazuri unayokuwa unayapata.
Na hilo ndiyo linakuvuruga na kukukatisha tamaa zaidi, maana unapoangalia juhudi unazoweka na matokeo unayopata haviendani.

Hapo unakuwa umepotezwa na vitu vidogo vidogo na visivyokuwa na tija.
Njia pekee ya kuondoka kwenye hilo ni kuweka vizuri vipaumbele vyako.
Katika mengi yanayokuja mbele yako, jua yapi ndiyo muhimu kwako kupata matokeo unayotaka.
Hayo pekee ndiyo unapaswa kuyapa kipaumbele na mengine kuachana nayo.

Unachopaswa ni kujua nini hasa unachotaka, kisha kufanya yale tu yanayokupa kile unachotaka.
Mengine yasiyohusika unaachana nayo kabisa, hupaswi kuyaruhusu yakuvuruge.

Na hata kwenye yale yanayochangia kile unachotaka, bado kuna ambayo yana mchango mkubwa kuliko mengine, hayo pia ndiyo unapaswa kuyapa uzito.

Muda, nguvu na umakini wako ni rasilimali muhimu na zenye uhaba.
Usikubali kuzipoteza kwenye mambo yasiyokuwa na tija kwako.

Sheria Ya Leo; Kumbuka kwamba udhibiti mkubwa wa mambo utatokana na kufanya tathmini halisia ya hali ilivyo, kitu kinachokuwa kigumu kama umezama kwenye mengi yasiyo na tija. Weka vipaumbele vyako vizuri na uhangaike na yale tu yenye tija kwako.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji