#SheriaYaLeo (301/366); Ona kivuli chako.

Kila mtu huwa ana pande mbili.
Upande mzuri ambao ndiyo anauonyesha kwa wengine.
Na upande mbaya ambao anauficha.

Wengi wakiwa hadharani hufanya mambo mazuri na ya kupendeza.
Lakini wakiwa faraghani hufanya mambo mabaya na yasiyo ya kupendeza.

Na mara nyingi, wale wanaojionyesha ni wema sana hadharani, huwa ndiyo wabaya zaidi faraghani.
Ile sehemu mbaya ya mtu huwa inakuwa na nguvu kubwa pale inapokandamizwa.
Hivyo mtu anapoikandamiza sehemu yake mbaya kwa kuonyesha zaidi sehemu nzuri, ndivyo sehemu hiyo mbaya inavyokuwa na nguvu na imara zaidi.

Hivyo njia ya kuvuka hilo siyo kuficha au kukandamiza sehemu mbaya, badala yake kuiona na kuijua.
Kutambua uwepo wake na wakati ambapo inataka kujidhihirisha ili uweze kuidhibiti.

Huwa inatokea unatamani kufanya kitu kibaya kwa mtu, au kutamani mwingine afikwe na mabaya.
Ukijaribu kukandamiza hilo kwa kuonekana ni mwema sana, unazidi kulipa nguvu na kusukumwa kufanya mabaya hayo ili nafsi yako iridhike.

Lakini kwa kutambua nguvu hiyo mbaya ya ndani na kuiona wazi, utaweza kuizuia isijidhihirishe.
Utatambua ni sehemu mbaya ya nafsi yako imeona hivyo, ambapo siyo lazima kutekeleza.

Usikane sehemu yako mbaya, kila mtu anayo. Ione na kuijua ili kuidhibiti isiwe na madhara kwako.

Sheria ya leo; Kupitia kujitambua wenyewe, tunaweza kupata njia ya kujumuisha upande wetu mbaya kwenye fikra zetu na kuidhibiti usilete madhara kwetu. Hilo litatufanya tuwe halisi kwetu na kuweza kutumia nguvu kubwa ya ndani yetu kuwa na ubunifu na uzalishaji mkubwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji