#SheriaYaLeo (309/366); Tumia wivu kama kichocheo cha mafanikio.

Pale unapokutana na watu wengine ambao wamepiga hatua kuliko wewe, kuna hali ya wivu huwa inakuingia.
Unaweza kuingiwa na hisia za kutaka kumuumiza au kumwibia.
Lakini hupaswi kujiruhusu kushuka chini kiasi hicho.

Badala yake pata tamaa ya kutaka kufanikiwa kama wao.
Pale unapokutana na wengine waliofanikiwa kuliko wewe, tamani na wewe ufanikiwe kama wao.
Kwa njia hiyo unakuwa umegeuza wivu wivu kuwa kichocheo cha mafanikio

Ili kuweza kukamilisha hilo, unahitaji mabadiliko yafuatayo ya kisaikolojia;
Kwanza unapaswa kuamini kwamba unao uwezo wa kufanikiwa kama walivyofanikiwa wengine. Kujiamini kwenye uwezo wako wa kujifunza na kuwa bora zaidi ndiyo dawa kuu ya wivu.
Badala ya kutamani kile ambacho wengine wanacho na kujaribu kuwahujumu, unaamua na wewe kupata kama hicho kwa sababu unajua uwezo kupata kama hicho unao.

Pili, unapaswa kujijengea nidhamu kali na imara ya kazi ili uweze kutumia kujiamini na uwezo wako kupata ulichopenda kwa wengine.
Kama tutajitoa kweli na kuwa na ung’ang’anizi, tutaweza kuvuka kikwazo chochote kile kinachoingia kwenye njia yetu.

Watu wavivu na wasio na nidhamu huwa ni rahisi kutawaliwa na hisia za wivu.

Sheria ya leo; Hatuwezi kuzuia hali ya kujilinganisha na wengine, ni asili yetu binadamu. Tunachoweza kufanya ni kuitumia hali hiyo kama kichocheo cha kufanya makubwa zaidi, kitu ambacho kinawezekana kama tutakuwa tayari kujifunza na kuweka kazi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji