2806; Tumbo la kuhara.
Kila mmoja wetu amewahi kukamatwa na tumbo la kuharisha.
Hii huwa siyo hali nzuri kwa sababu ya maumivu makali na hitaji la kwenda choo mara kwa mara.
Hakuna anayeipenda hii hali.
Wote tunajua sababu kuu ya tumbo la kuhara. Huwa inasababishwa na kula kitu ambacho siyo safi.
Pamoja na kwamba ulaji ndiyo umeleta shida hiyo kubwa, bado hatuachi kula, hata wakati huo huo ambapo tumbo linatuuma.
Tunachofanya ni kuwa na tahadhari kwenye kile tunachokula. Tunahakikisha tunakula kwenye hali ya usafi ili tusipatwe tena na tumbo la kuhara.
Tunajua pamoja na kwamba kuhara kumesababishwa na kula, hatuwezi kususa kula, maana huo ndiyo uhai.
Sasa tuliangalie hili kwenye maeneo mengine.
Umepanga kutembelea au kuwapigia simu wateja wa biashara yako.
Katika zoezi hilo mteja mmoja anakujibu vibaya na kukudhalilisha.
Nini kinachotokea?
Unaahirisha kabisa zoezi zima. Unajiambia hutapiga tena simu wala kutembelea wateja.
Yote hiyo kwa sababu ya mteja mmoja au wachache ambao wamekukwamisha.
Ni sawa na kujiambia hutakula tena kwenye maisha yako kwa sababu umeharisha!
Au umeweka malengo na mipango fulani na pale unapoanza kuchukua hatua unakutana na vikwazo.
Na hapo hapo unaamua kuachana kabisa na malengo na mipango yako yote kwa sababu ya vikwazo hivyo.
Rafiki, hakuna kilichonyooka kwenye maisha, hakuna kinachoenda kama ulivyopanga wewe.
Kila kitu huwa kinakutana na vikwazo na changamoto.
Ukiwa mtu wa kususa kila unapokutana na hayo magumu, kamwe hutaweza kufanikiwa.
Kimafanikio utakufa njaa kama mtu aliyesusa kula baada ya kuhara.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kuwa umeshajua kile unachotaka na kwa kuwa unajua unachopaswa kufanya ili kukipata, basi fanya maamuzi kwamba utafanya mpaka upate. Haijalishi umekutana na magumu na vikwazo kiasi gani, endelea kufanya kama ulivyopanga. Usisuse wala kukata tamaa. Badala yake angalia namna ya kufanya kwa ubora zaidi.
Tafakari;
Mafanikio yangekuwa rahisi kila mtu angekuwa nayo.
Lakini siyo rahisi ndiyo maana wengi hawana.
Unapokutana na ugumu kwenye safari yako ya mafanikio jua upo njia sahihi, kwani ugumu huo unawapunguza wale ambao hawajajitoa kweli kupata kile wanachotaka.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed