2807; Unahangaika na mambo mengi sana.

Mwanga wa jua, ukitawanyika, unaishia kuangaza tu.
Lakini mwanga huo huo ukikusanywa sehemu moja, unakuwa na nguvu ya kuchoma.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye nguvu zetu binafsi, tukizitawanya kwenye mambo mengi, tunaishia kupata matokeo ya kawaida.
Lakini tukikusanya nguvu hizo kwenye jambo moja au machache, matokeo tunayoyapata yanakuwa makubwa sana.

Watu wamekuwa wanalalamika hawana muda au hawapati matokeo mazuri licha ya kuweka juhudi kubwa.
Lakini ukiangalia kwa kina, unagundua kuna mambo mengi yasiyokuwa na tija ambayo wanahangaika nayo.

Tambua, kitu chochote kinachochukua nguvu au muda wako, ambacho hakihusiani na mafanikio yako, ni kikwazo kwenye mafanikio yako.

Unakuwa umetawanya sana nguvu zako kiasi kwamba matokeo unayokuwa unayapata ni madogo ungelinganisha na yale ambayo ungeweza kupata kama usingekuwa umetawanya nguvu hizo.

Kama unaendesha gari, ukikanyaga mafuta gari inapaswa kuongeza mwendo. Kama unakanyaga mafuta na gari haiongezi mwendo, maana yake pia umekanyaga na breki.

Breki kwako ni mambo yote unayohangaika nayo ambayo hayana mchango kwenye mafanikio yako.
Na siyo tu kwenye mambo unayofanya, bali hata unayofikiria.
Chochote kinachokupa hofu kinapunguza kasi yako kwenye yale unayofanya.

Kama unataka kupata mafanikio makubwa kwa uhakika kwenye maisha yako, achilia kabisa breki zote unazojiwekea.
Anzia kwenye fikra zako, ondokana na fikra zote za kushindwa au kuhangaika na mengine yasiyo na tija.
Nenda kwenye hisia, achana na hisia zote hasi za hofu, wivu, chuki na kukata tamaa. Hizo hazina mchango zaidi ya kukurudisha nyuma.

Halafu pitia kwenye roho, achana na imani zozote ambazo zinakuwa kimwazo kwa mafanikio yako.
Na funga kazi ni kwenye mwili, chochote unachotaka kufanya, jiulize kinachangiaje wewe kufika kule unakotaka kufika.
Kama hakina mchango, achana nacho kabisa. Hakuna haja ya kufanya kitu kisichokuwa na mchango kwenye mafanikio yako.

Kwenye maisha, rasilimali zote muhimu na tunazozihitaji sana huwa zina ukomo. Hivyo tunahitaji kuwa na vipaumbele vikubwa katika kuzitumia rasilimali hizo kama tunataka kupata matokeo bora.

Mafanikio siyo tu kufanya na kuwa bize, bali kufanya yale yaliyo sahihi.

Hatua ya kuchukua;
Chukua kalamu na karatasi. Igawe karatasi hiyo kwenye pande mbili. Upande mmoja andika malengo unayotaka kuyafikia. Upande wa pili andika mambo yote uliyofanya ndani ya siku 7 ambazo zimepita. Kisha oanisha kila ulilofanya na malengo unayotaka kufikia.
Chochote ambacho ulifanya na hakina mchango kwenye lengo lolote, acha kukifanya mara moja. Ni vitu vya aina hiyo ambavyo vinakurudisha nyuma na kukuzuia usifanikiwe.

Tafakari;
Ili uweze kupata matokeo ambayo ni tofauti na yale unayopata sasa, unapaswa kufanya tofauti na unavyofanya sasa.
Kama kuna mahali umekwamba, umejikwamisha na mahangaiko yako kwenye mambo yasiyokuwa na tija.
Badili vipaumbele vyako na utashangaa jinsi matokeo yako yatakavyobadilika.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed