2808; Kujua hujui.

Kujua hujui ndiyo ujuzi muhimu ambao utakusaidia sana kwenye maisha yako.
Utakufanya uwe mnyenyekevu na tayari kujifunza ili kuwa bora zaidi na kuweza kupiga hatua kubwa.

Na hili siyo rahisi kukubali na hata kulifanya.
Huwa tuna ufahari wa kutaka kuwaonyesha wengine kwamba tunajua.
Huwa tunaona kuonekana hatujui ni ujinga mkubwa.
Hivyo tunajifanya tunajua, hata kama hatujui.

Matokeo yake ni kuumbuliwa na yale tusiyoyajua.
Yanatupelekea kukutana na magumu na changamoto ambazo zinakuwa kikwazo kikubwa kwetu.
Kitubambacho kingekuwa rahisi kama tungekubali tu hatujui na tukajifunza.

Kila anayejua kitu leo, alijifunza.
Hakuna yeyote aliyezaliwa akiwa anajua kitu chochote.
Hivyo hakuna ubaya kutokujua.
Lakini kujifanya unajua wakati hujui, kuna ubaya mkubwa.
Kwani unatengeneza matatizo ambayo yatakusumbua sana.

Vitu unavyojua mpaka sasa ni vichache sana ukilinganisha na vile ambavyo huvijui.
Hivyo kama kuna hatua hupigi, huenda kukwama kwako kunaanzia kwenye yale ambayo hujui.
Kwa kujifanya unajua, unakuwa unazidi kujichelewesha kupiga hatua.

Hatua ya kuchukua leo.
Fikiria kule unakotaka kufika, ambapo bado hujafika.
Kisha anza kuorodhesha ni vitu gani hujui ambavyo vinakukwamisha kufika huko?
Anza kufanya kazi ya kujifunza hivyo ambavyo bado hujavijua ili uweze kutoka hapo ulipokwama sasa na kupiga hatua kubwa zaidi.

Tafakari;
Kila mtu ni mjinga kwenye mambo fulani, lakini ujinga huisha pale mtu anapojifunza kile asichokijua.
Tatizo lipo kwenye upumbavu, ambapo mtu hajui, lakini anajifanya anajua. Kwa njia hiyo hawezi kujifunza, hivyo anazidi kubaki pale alipo na kutokupiga hatua yoyote ile.
Usiwe mpumbavu, kubali yale ambayo hujui na ujifunze.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed