#SheriaYaLeo (319/366); Igiza chenye ushawishi.

Katika nyakati zozote tunazoishi, huwa kuna tabia fulani ambazo huwa zinaonekana chanya na kukubalika na wengine.
Hizo ndizo tabia unazopaswa kujua jinsi ya kuzionyesha ili ukubalike na wengine na uwe na ushawishi.

Kwa mfano, kuonekana mtakatifu kwa nje ni kitu ambacho hakijawahi kupitwa na wakati.
Kuonekana mtakatifu kunafanya ukubalike na wengi.
Kwa zama hizi, utakatifu ni kuonekana mpenda maendeleo, mwenye uvumilivu na mwenye fikra za wazi.
Inabidi uonekane ukitoa misaada kwa wenye uhitaji na kuunga mkono mambo ya aina hiyo wazi wazi.

Kuonyesha tabia ya uaminifu pia kuna ushawishi mkubwa. Kukiri baadhi ya madhaifu yako kwa wengine kutawafanya wakuone ni mnyenyekevu na mwenye uaminifu.

Yote hayo siyo lazima yawe halisi kwako, kuweza kuyaigiza vyema kunawafanya watu wakuamini na kushawishika na wewe.

Hivyo mara zote igiza tabia zenye ushawishi na igiza kwa namna ambayo watu hawataona unaigiza.
Wafanye waone ndiyo tabia halisi kwako na hilo litawafanya wakukubali na kushawishika na wewe.

Sheria ya leo; Kama watu wanawahukumu wengine kwa mwonekano wa nje, jifunze jinsi ya kudhibiti mwonekano wako ili ukubalike na wengine na uwe na ushawishi kwao. Kuonekana mtakatifu na mnyenyekevu kuna ushawishi mkubwa. Muhimu ni kuhakikisha huonekani ukiigiza au ukiwa mnafiki.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji