#SheriaYaLeo (322/366); Linganisha ubunifu na uhalisia.

Chochote unachofanya, huwa kinaanza na mawazo yako ya kibunifu. Kadiri unavyokwenda unakazana kuwa na ubunifu zaidi ili kufanya kitu cha tofauti.

Unapoanza kufanya kulingana na mawazo yako ya kibunifu, kuna matokeo unayoyapata na mrejesho kutoka kwa wengine.
Hapa unahitaji sana kupata maoni ya wengine kulingana na unachofanya na matokeo unayopata.
Unataka kusikia makosa ya kile unachofanya ili uweze kukiboresha zaidi.

Kama unachofanya kinashindwa, matokeo yamekuja tofauti au tatizo limeshindwa kutatuliwa, unapaswa kuchukulia kama sehemu nzuri ya kujifunza.
Jua kipi umekosea kufanya, jichunguze kwa kina na kweli.

Baada ya kupata mrejesho, unakwenda kufanya tena, ukitumia mrejesho uliopata, pamoja na mawazo yako ya kibunifu.
Unaendelea na mzunguko huo mpaka kupata matokeo mazuri unayoyataka.

Ni muhimu utumie vyote, mawazo yako ya kibunifu na mrejesho wa wengine ndiyo uweze kuzalisha matokeo bora.
Ukikazana na mawazo yako ya kibunifu pekee, utakachozalisha hakitaendana na uhalisia.
Na ukikazana na mrejesho wa wengine tu, unachozalisha kitakuwa cha kawaida sana na hakitakuwa na utofauti wowote.

Ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa mawazo yako ya kibunifu na mrejesho wa wengine, kuvitumia pamoja ili kuzalisha matokeo bora, ya kipekee lakini pia yanayoendana na uhalisia.

Sheria ya leo; Kwa kutumia mawazo yako ya kibunifu na mrejesho kutoka kwa wengine, unachozalisha kibakuwa cha kipekee, lakini pia kinachoendana na uhalisia wa wale unaowalenga.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji