2819; Umechagua mwenyewe.
Hakuna jambo linaloshangaza kwenye maisha kama hili, watu kulalamikia na kulaumu wengine kwa machaguo yao wenyewe.
Kwa zama tunazoishi sasa, hakuna yeyote anayekulazimisha kufanya chochote. Ni wewe mwenyewe umechagua.
Chukua mfano wa mtu anayefanya kazi na analipwa mshahara kidogo. Anaweza kumlaumu mwajiri wake kwa kutokumjali, lakini hayo ni machaguo yake mwenyewe.
Ni yeye amechagua kufanya kazi hiyo inayomlipa kidogo, hakuna anayemlazimisha.
Lakini pia ni yeye amechagua kufanya kazi ya thamani ya chini, ambayo mwajiri ana nguvu ya kulipa kidogo na asiathirike.
Kama mtu huyo angekuwa na thamani kubwa ambayo mwajiri anaitegemea sana na hataki kuipoteza, angelazimika kumlipa zaidi ili asimkose.
Huo ni mfano mmoja, lakini kila ukichonacho au kinachotokea kwenye maisha yako, ni zao la machaguo yako mwenyewe.
Aina ya biashara unayofanya, wateja ulionao na faida unayotengeneza, yote inatokana na machaguo ambayo umefanya huko nyuma.
Tuchukulie kitu kimoja ambacho wengi wanakilalamikia sana, muda. Karibu theluthi mbili ya muda wako unaudhibiti wewe mwenyewe. Hivyo kama huna muda wa kufanya mambo unayotaka kufanya, siyo kwa sababu ya mtu mwingine yeyote anayechukua muda wako, bali ni kwa sababu ya machaguo yako binafsi kwenye kutumia muda.
Kila unachopanga kufanya na muda wako, hata kiwe kidogo kiasi gani, kinaathiri muda na matokeo yako.
Tuseme pia kuna mtu amekudanganya, kukutapeli au kukuibia. Unaweza kuona watu hao wanastahili lawama. Lakini ni wewe mwenyewe unayekuwa umechagua kuwaamini au kuwaonyesha na kuwapa fursa ya kuweza kukuibia.
Chochote kile kinachotokea kwenye maisha yako, ni matokeo ya machaguo yako mwenyewe.
Ukitaka kuyabadili maisha yako, unapaswa kuanza kwa kubadili machaguo unayoyafanya.
Kumbuka upo huru kuchagua, tumia uhuru huo kwa manufaa yako.
Wajibika na maisha yako, usipende kulalamika na kulaumu kwa mambo ambayo umeyachagua wewe mwenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Chukua uwajibikaji mkubwa wa maisha yako. Kwa chochote kinachotokea kwenye maisha yako, iwe kizuri au kibaya, tambua ni matokeo ya machaguo yako huko nyuma. Hivyo badala ya kulalamika au kulaumu, angalia ni machaguo gani bora zaidi unayopaswa kufanya leo ili uyabadili matokeo ya kesho.
Tafakari;
Kulalamika na kulaumu ni rahisi, lakini kuwajibika ni kugumu.
Unajua chochote rahisi huwa kinakimbiliwa kufanywa na wengi na hakina thamani.
Hivyo wewe ondokana kabisa na kulalamika na kulaumu, badala yake wajibika na maisha yako.
Miliki matokeo unayopata na fanya machaguo bora zaidi ili kupata matokeo bora.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed