#SheriaYaLeo (323/366); Angalia nje yako pia.
Kwa asili sisi binadamu huwa tunajiangalia sisi wenyewe zaidi. Huwa tunajali zaidi kuhusu changamoto zetu na matakwa yetu pia.
Wewe unapaswa kwenda kinyume na hili kadiri iwezekanavyo.
Na utaweza kulifanya hilo kwa njia tatu;
Kwanza unakuwa msikilizaji makini.
Unaweka umakini wako wote kwa wengine, kusikiliza kwa umakini mkubwa siyo tu kwa masikio, bali kwa macho pia.
Unajifunza kuelewa maana ya yale ambayo watu wanasema.
Unazielewa hisia za watu, hata zile ambazo wanajaribu kuzificha.
Umakini kwenye kuwasikiliza watu utakuwezesha kupata vitu vingi kutoka kwao.
Mbili unajitoa kuhakikisha watu wanakuheshimu. Huchukulii kwamba ni wajibu wao kukuheshimu kwa sababu ya nafasi yako au ukuu wako.
Watu wanakuheshimu pale unapoheshimu matakwa yao binafsi na kuonyesha kwamba unafanyia kazi kuboresha maslahi yao.
Unawafanya watu waone upo kwa ajili yao na hilo linawafanya wakuheshimu sana.
Tatu unachukulia kuwa kiongozi ni wajibu mkubwa mwako, maslahi ya kundi zima yakitegemea kwenye kila maamuzi unayofanya.
Kinachokusukuma siyo kupata sifa, bali kuleta matokeo bora kwa watu wengi zaidi.
Unazama kwenye kufanya kazi na siyo majigambo. Unapata hisia za kuwa na muunganiko mkubwa na kundi hilo, ukiona hatima yako na yao zikiwa zimeungana.
Sheria ya leo; Ukiwa na mtazamo huu wa kuangalia nje na kujali maslahi ya wengine, watu watavutiwa zaidi kuja kwako, kwa sababu utakuwa wa kipekee sana kujali mambo ya wengine na kuegemea kwenye matokeo mazuri.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji