#SheriaYaLeo (326/366); Ungana na kilicho karibu yako.

Maisha ni mafupi na nguvu zetu zina ukomo.
Kwa kuongozwa na tamaa zetu, tunaweza kupoteza muda na nguvu kwenye kutafuta mabadiliko.

Kwa ujumla, hupaswi kusubiri na kutumaini mambo yatakwenda vizuri, bali unapaswa kutumia vizuri kile ulichonacho.

Asili inakuunga mkono. Kwa kuzamisha akili yako kwenye kile kilicho karibu yako zaidi, badala ya vilivyo mbali, inakuletea hisia tofauti.

Kwa watu walio karibu yako, unaweza kujenga nao mahusiano ya kina. Kuna mengi ambayo bado hujayajua kuhusu watu hao, hivyo wana mengi ya kukushangaza.

Unaweza kuungana kwa kina na mazingira yako. Eneo ambalo upo, lina historia kubwa ambayo bado huijui. Kwa kuyajua mazingira yako vizuri kunafungua fursa nyingi kwako.

Hata kwako mwenyewe, kuna vitu vingi ndani yako ambavyo bado hujavielewa kwa kina. Kwa kukazana kujijua wewe mwenyewe kwa kina, utaweza kutawala asili yako badala ya kutawaliwa nayo.

Kazi au biashara unayofanya pia ina maeneo mengi ambayo unaweza kuyaboresha zaidi. Lakini ni mpaka uzame kwa kina zaidi ndiyo utaweza kuyaona na kuyafanyia kazi.

Una mengi yaliyo karibu yako ambayo unaweza kuyafanyia kazi ukawa bora kabla hujaanza kuhangaika na yale yaliyo mbali na ambayo huwezi kuyafikia kwa uhakika.

Sheria ya leo; Mwisho wa siku, kitu unachopaswa kuhangaika nacho zaidi ni kujenga mahusiano ya kina na uhalisia unaokuzunguka. Kufanya hivyo kutakuletea utulivu, umakini na nguvu za kuweza kubadili yale yanayoweza kubadilishwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji