2823; Tayari najua.

Hayo ni maneno ambayo yamewapoteza wengi sana na kuwazuia wasifanikiwe.

Ni maneno ambayo yamewazuia wengi wasiendelee kujifunza na kuwa bora zaidi.

Kila mtu hudhani tayari anajua mengi, lakini kiuhalisia hana uelewa kama anavyodhani anao.

Kujifunza kitu chochote kile, kunahitaji marudio ya muda mrefu.
Hata pale unapodhani tayari unajua, bado yapo mengi ambayo unaweza kuendelea kujifunza.

Kuna kitu kipya utakachojifunza kwa kuwa tayarj kujifunza kwenye kila kitu bila kujiambia tayari unajua.

Kila fursa ya kujifunza ina kitu cha tofauti ndani yake, hata kama ni kitu ambacho tayari mtu unajua.

Hii safari ya mafanikio ni ya kujifunza endelevu na kwa kurudia rudia.
Kuna mambo ya msingi ambayo utaendelea kujifunza na kufanyia mazoezi mara kwa mara ili uzidi kuwa bora.

Kila unapokutana na kitu au hali unayojiambia tayari unajua, jipe changamoto. Jiambie kuna kitu cha tofauti bado hujakijua, hivyo weka umakini wako wote kwenye kitu hicho ili ujifunze na kukifanya kwa ufanisi mkubwa.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapokutana na kitu au hali ya kujifunza, usijiambie tayari unajua. Badala yake jiulize unawezaje kujifunza na kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa kabla.
Utakachoona kitatokana na fikra zinazokutawala.
Ukitaka kuona fursa za kujifunza utaziona na kuweza kuzitumia.
Kadhalika ukiona tayari unajua, hakuna kipya cha kujifunza utakachoweza kukiona.

Tafakari;
Hakuna chochote utakachojifunza ukatoka ukiwa huna chochote kipya.
Hata yale unayoona tayari unayajua, bado kuna mengi unaweza kujifunza.
Hivyo kila mmoja anapaswa kuwa na utayari wa kujifunza kwenye kila anachokutana nacho, hata kama ni cha kawaida kabisa.
Futa maneno TAYARI NAJUA na badala yake tumia KUNA CHA KUJIFUNZA.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed