2825; Unamtoa mtu.

Kwenye maisha, kila mtu tayari ana mtu wake.
Hivyo unapotaka kupata mtu, inabidi uwe tayari kumtoa aliyepo.

Twende kwenye mfano ili tuelewane. Kama upo kwenye biashara, wateja unaowalenga tayari wana pengine wanaponunua hicho unachouza.
Ili uwapate waje kununua kwako, lazima uwatoe kule walipo sasa.

Siyo rahisi kumtoa mtu kwenye kile ambacho ameshakiamini na kukizoea.
Ni kitu kinachokutaka wewe ujenge thamani kubwa na kuaminika zaidi.
Inakutaka uwe na uvumilivu na ung’ang’anizi mkubwa.

Hata kama mteja anakuambia tayari anaridhishwa na kule anakopata huduma/bidhaa, usiache kumfuatilia.

Kuna siku huyo anayemtegemea atamkwamisha, siku ambayo mteja huyo atakasirishwa na hilo. Hiyo ndiyo itakuwa siku nzuri kwako kupata nafasi ya kumpa kile alichokosa na kumteka akawa mteja wako.

Kama mteja hajafa, usimfute kwenye mpango wako wa ufuatiliaji. Kuna upenyo unaweza kupatikana na ikawa fursa nzuri kwako kumpata mteja huyo, hata kama alishakuambia tayari ana mtu wake.

Hatua ya kuchukua;
Orodhesha wateja wote ambao ungependa sana wawe wateja wako, lakini kwa sasa tayari wanahudumiwa pengine ambapo wanapafurahia. Waweke kwenye mchakato wa kuwafuatilia na waendelee kusikia kutoka kwako mara kwa mara. Siku ambayo yule wanayemtegemea anawakwamisha, wewe unapata fursa.

Tafakari;
Kwenye maisha kila mtu tayari ana mtu wake. Kwa watu unaowataka, tafuta sababu ya wao kuwa tayari kuwaacha walionao na wakakukubali wewe. Kwa njia hiyo utaweza kuwapata wengi utakavyo.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed