2826; Mkato mzuri.
Njia za mkato huwa siyo nzuri kwenye maisha.
Kwani zimekuwa ndiyo chanzo cha wengi kukosa yale wanayotaka.
Watu wamekuwa wanahangaika na njia nyingi za mkato, lakini wanaishia kupoteza muda, nguvu na hata fedha.
Huwa kuna usemi lifti ya kuelekea kwenye mafanikio imeharibika, inabidi upande ngazi.
Lakini kuna kitu kimoja ukitumia njia ya mkato kitasaidia sana.
Kitu hicho ni kuangalia wingi wa watu wanaokikimbilia kitu.
Ukisikia kuna fursa nzuri ya mafanikio na kila mtu anaielewa na kuikimbilia, kaa mbali. Hakuna fursa hapo.
Hii ndiyo njia pekee ya mkato ambayo unaweza kuitumia na ikakuepusha kupoteza muda kwenye maisha yako.
Chochote kinachokimbiliwa na wengi huwa hakina ugumu sahihi wa kukifanya kimpe mtu mafanikio.
Kitendo tu cha wengi kukimbilia, ni kiashiria cha wazi kwamba hata ushindani nao utakuwa mkali pia.
Kuna mengi makubwa na mazuri ya kufanya kwenye maisha.
Ili usipoteze muda na nguvu kwa yasiyo sahihi, angalia wingi wa watu wanaokimbilia kitu.
Ukishaona wengi wanakikimbilia, usiungane nao, wewe nenda kwenye kitu kingine.
Labda kama wengi hao wamekukuta wewe kwenye kitu hicho, hapo ndiyo utafanikiwa sana kwa kutangulia.
Tumia wingi wa watu kama chujio la haraka ili uepuke kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa sahihi kwako.
Hatua ya kuchukua;
Angalia fursa zote ambazo zilikuwa zinakimbiliwa na kila mtu. Baada ya muda zote zilipasuka na watu kuingia hasara kubwa.
Tumia wingi wa watu kama kigezo cha kupima usahihi wa fursa kwako.
Tafakari;
Huna muda wa kuchunguza kila fursa kwa undani wake ili kujua kama ni sahihi au la. Maana fursa ni nyingi na zote zinavutia.
Kurahisisha hilo la kuchuja, angalia wingi wa watu wanaoikimbilia fursa husika.
Unapoona fursa inakimbiliwa na wengi, hiyo ni sababu ya kutosha ya kuiepuka, haiwezi ikawa sahihi kwako.
Wengi wanapenda urahisi na hakuna mafanikio yamewahi kutokana na urahisi.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed