#SheriaYaLeo (334/366); Mwendeshaji na farasi.

Uhusiano kati ya fikra na hisia zetu ni kama mwendesha farasi na farasi.
Hisia zetu ni farasi na fikra zetu ni mwendesha farasi.

Farasi ana nguvu kubwa, lakini bila ya kuongozwa vyema anaishia kuzunguka huku na huko na kutokuleta matokeo yoyote yenye tija.
Hivyo ndivyo hisia zetu zilivyo, zisipoongozwa vyema, zinaishia kutupeleka kwenye mambo yasiyokuwa na manufaa.

Mwendesha farasi ana udhibiti mkubwa, lakini bila ya nguvu, hawezi kuenda popote.
Hivyo ndivyo fikra zetu zilivyo, zinaweza kufikiri mengi na kufanya maamuzi, lakini bila ya hisia hakuna hatua zinazoweza kuchukuliwa.

Hisia na fikra ni lazima vifanye kazi kwa kushirikiana vizuri. Fikra zifanye maamuzi sahihi na kisha hisia zitekeleze maamuzi hayo.
Hivyo ndivyo mtu anavyoweza kufanya makubwa kwenye maisha yake.

Tatizo la wengi hutawaliwa na hisia, kusukumwa kuchukua hatua kwa hisia bila kufikiri kwa usahihi. Hilo huwapelekea kufanya maamuzi mabovu na ambayo yanawagharimu.

Wengine wanakuwa na udhibiti mkali wa kifikra na kuziweka pembeni kabisa hisia. Wanakuwa na maamuzi mazuri lakini hakuna wanachofanya.

Ili ufanye makubwa, lazima kuwe na mlinganyo chanya wa fikra na hisia. Ufikiri kwa kina na kuamua, kisha uyatekeleze maamuzi kwa hisia.

Sheria ya leo; Hatuwezi kutenganisha hisia na fikra, ni vitu ambavyo vina mwingiliano mkubwa. Kila mtu ana kimoja kilichotawala, wengi hisia, baadhi fikra. Jifunze kuvitumia vyote kwa pamoja na utaweza kufanya makubwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji