#SheriaYaLeo (336/366); Ulimwengu wa kushangaza na usio na ukomo.

Ulimwengu ni wa kushangaza na usio na ukomo.
Katika kulielewa na kulisimamia hilo, jamii mbalimbali zimekuwa na tararibu zake.
Ni taratibu ambazo zinalenga kuwafanya watu waweze kuyathamini maisha yao hapa duniani.

Matambiko, ubatizo na hata taratibu nyingine za kimila, kifalsafa na kidini, zinalenga kufanya watu watambue jinsi ulimwengu ulivyo wa kushangaza na usio na ukomo.
Kipindi cha nyuma, watu hawakuwa na njia ya kuweza kuelewa baadhi ya mambo yaliyokuwa yanatokea.
Hivyo kulikuwa na hatua zilizowasaidia watu kuendana na yote yaliyokuwa yanaendelea.

Lakini kwa zama hizi, mambo yamebadilika. Tunaona kama baadhi ya taratibu ambazo watu wa zamani walikuwa wanafanya ili kuielewa dunia zimepitwa na wakati.
Hiyo imepelekea tupuuze mambo hayo na kuyaacha.

Kibaya ni kwamba tumeishia kutekwa na mambo madogo madogo na yasiyo na tija yanayoendelea kwenye maisha ya kila siku.
Kweye zama hizi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimeteka umakini wetu na kutuzamisha kwenye mambo madogo madogo na yasiyo na tija.

Hilo linatufanya tushindwe kuona na kuthamini ulimwengu usio na ukomo na wa kushangaza.
Kushindwa kuona hilo, kunayafanya maisha yakose msingi imara na watu kuwa rahisi kuyumbishwa na mambo yasiyokuwa na tija.

Kama mtu unataka kuondokana na hadaa hiyo ya zama hizi n kuweza kutambua na kudhamini ukubwa wa ulimwengu, ni lazima ufanye mambo ambayo ni kinyume na wengi wanavyofanya.

Lazima ujitenge na usumbufu unaoendelea na upate nafasi ya kukaa kwenye ukimya, kusali, kufanya tahajudi na mengine yanayokuunganisha na ulimwengu mkubwa usio na ukomo.

Ifanye akili yako kuiona picha kubwa ya ulimwengu wa kushangaza na usio na ukomo. Hilo litakupa utulivu mkubwa na kuyaelewa baadhi ya mambo yanayotokea, ambayo hayana maelezo ya moja kwa moja.

Sheria ya leo; Iondoe akili yako kwenye usumbufu unaoendelea sasa na kaa kwenye utulivu wa kuweza kuelewa ulimwengu wa kushangaza na usio na ukomo. Hiyo itakuwezesha kuyaelewa mengi na kuweza kuyatumia vizuri.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji