2833; Ni bora kuliko.

Huwa siishiwi kushangazwa na jinsi ambavyo watu wanaotumia njia zinazowakwamisha, wanakataa njia mpya kwa sababu haina matokeo ya asilimia moja.

Chukua mfano unafanya biashara na huna mikakati yoyote ya masoko na mauzo na hivyo mauzo yako ni ya kawaida sana.
Unafundishwa mkakati bora wa masoko na mauzo, lakini unakataa kuutumia kwa sababu haufanyi kazi kwa asilimia 100. Je hapo unanufaikaje?

Kwa mfano kama hupigii kabisa wateja wako simu na unauza laki 1 kwa siku.
Ukapewa mkakati wa kupigia simu wateja10 kila siku.
Katika hao 10, 8 wanakataa kununua, ila wawili wanakubali kununua na mauzo yanakuwa laki 1 na elfu 20.

Unakataa mpango huo wa simu, kwa kusema haufanyi kazi, kwa sababu watu 8 kati ya 10 wamekataa.
Unabaki na laki moja yako ya kubahatisha. Je huoni hapo unajikwamisha mwenyewe?

Kitu chochote kipya unachojifunza, ambacho kina uwezo wa kukupa matokeo zaidi ya yale unayopata sasa, hata kama tofauti ni ndogo, kitu hicho ni bora kuliko unachofanya, hivyo unapaswa kukifanya.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jifunze, dadisi na jaribu njia za kukiboresha zaidi. Kama kuna matokeo bora yanaweza kupatikana, hata kama ni madogo, fanya. Usiangalie kushindwa kulikopo, wewe angalia matokeo ya tofauti unayokwenda kupata.

Tafakari;
Usisubiri mpaka upate kitu chenye uhakika wa asilimia 100 ndiyo ufanye. Wewe angalia matokeo ya tofauti yanayoweza kupatikana, kama yapo basi fanya. Kufaulu mtihani siyo mpaka upate 100, hata 50 ni ufaulu mkubwa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed